2016-02-02 10:44:00

Watawa pyaisheni maisha yenu kwa kujikita katika karama, maisha na ushuhuda!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakuzungumzia kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yanayofikia kilele chake kwa Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari. Hii pia ni Siku ya 20 ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Watawa wanaadhimisha pia Jubilei inayowachangamotisha kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika huduma mbali mbali za maisha ya mwanadamu!

Askofu mkuu Ruwa'ichi anasema kwamba, familia ya Mungu katika  maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani imepata nafasi ya kutafakari, kushukuru, kusali na kuadhimisha zawadi ya maisha ya wakfu katika Kanisa sanjari na kuungana na watawa katika kuwaenzi katika maisha na majitoleo yao kwa maisha na utume wa Kanisa katika medani mbali mbali za maisha. Imekuwa ni nafasi ya kuadhimisha uwepo, ufuasi na utume wa watawa ndani ya Kanisa.

Waamini wamepata nafasi ya kusali kwa ajili ya kuombea miito ya upadre na maisha ya kitawa, ili Kanisa liweze kupata watendakazi watakatifu, waadilifu na wachapakazi, tayari kujisadaka kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake, wakitambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Watawa pia wamepata nafasi ya kutafakari kuhusu: maisha, utume, karama, changamoto na fursa mbali mbali, tayari kujipyaisha ili kujenga na kuimarisha utume na maisha ya Kanisa zima.

Changamoto kubwa iliyojionesha ni ufinyu wa uelewa wa maisha ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa hususan kuhusiana na maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, baadhi ya waamini walidhani kwamba, Mwaka wa Watawa ni kwa ajili ya watawa peke yao na waamini walei hawahusiki kwa lolote lile! Ikumbukwe kwamba, watawa ni wanakanisa, kwa ajili ya Kanisa pamoja na Kanisa. Hapa familia ya Mungu inapaswa kufundwa barabara ili kutambua na kuthamini maisha, wito na utume wa watawa ndani ya Kanisa, tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima.

Waamini walei waendelee kuonesha mshikamano wa hali na mali na watawa sehemu mbali mbali za dunia. Watawa nao kwa upande wao, waendelee kutafakari maisha na utume wao, ili kujikita katika mchakato wa kujipyaisha. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani iwe ni chachu ya kupyaisha maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa kwa kujikita katika zaidi katika wakfu, utume na ushuhuda. Watawa wajitahidi kutamadumisha na kumwilisha karama za Mashirika yao katika maisha na utume wa Makanisa mahalia; ili waweze kutakatifuzwa, kumtukuza na kulifaidisha Kanisa. Askofu mkuu Ruwa'ichi anawaalika wanafamilia ya Mungu popote pale walipo kusaidia kuenzi na kudumisha tunu za maisha ya kitawa, kwani Kanisa bila watawa ni dhaifu. Karama mbali mbali za Mashirika ya kitawa zinalipamba Kanisa na kumshuhudia Kristo Yesu pamoja na Injili yake kwa watu wa mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.