2016-02-02 07:39:00

Papa "Wambea hawana bunge na wala umbea si mtaji wangetajirika wengi"


Maadhimisho ya kufunga Mwaka wa Watawa Duniani, Jumatatu tarehe Mosi Februari 2016 yalichukua sura mpya pale Baba Mtakatifu Francisko alipokabidhi hotuba yake kuhusu wosia ambao amependa kuwakabidhi watawa wakati huu Mama Kanisa anapofunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani kwa kuwataka wayakite maisha yao katika mambo makuu matatu: Unabii, Ujirani na Matumaini. Baba Mtakatifu akaamua kutoa katekesi ya kina kwa kuzungumza na watawa moja kwa moja, ili kuangalia ukweli wa maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, watawa katika maisha na utume wao ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu, Kanisa na jirani, huku wakiyasimika maisha yao katika Mashauri ya Kiinjili, yaani: ufukara, utii na useja kama alivyofanya Kristo mwenyewe. Unabii unajikita katika majadiliano na utii, daima kwa kutafuta kutenda na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha ya kitawa na wala si kwa ajili ya kujitafuta mwenyewe au kufanya kila ambacho mtawa anajisikia kutenda.

Unabii ni ushuhuda unaowaonesha watu njia ya furaha na ukuu unaofumbatwa kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni zawadi ya Roho Mtakatifu, mwaliko kwa watawa kutofanya wala kuishi kwa mazoea. Watawa wanahimizwa na Baba Mtakatifu kuwa kweli ni manabii kwa kusema kile ambacho anatakiwa kusema na kutenda kwa wakati muafaka, ili maisha yote ya mtawa yawe ni ushuhuda wa kinabii, wenye kuleta mvuto na mashiko kwa watu wanaowazunguka.

Baba Mtakatifu anawataka watawa kujenga na kudumisha utamaduni wa ujirani mwema, ili kubomoa kuta za utengano na badala yake kujenga madaraja ya watu kukutana na kuonja tunu msingi za maisha ya Kikristo; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa wajitahidi kuwa karibu na jirani zao: kiroho na kimwili; hususan kwa njia ya huduma makini. Ujirani mwema anakaza kusema Baba Mtakatifu unapaswa kupata chimbuko lake katika maisha ya kijumuiya. Watawa waondokane na tabia ya “kupika majungu kwani wambea hawana bunge na wala umbea si mtaji, ungekuwa mtaji wengi wangetajirika”.

Umbea ni sawa na ugaidi katika maisha ya kijumuiya, changamoto ya kuondokana na tabia kama hizi zinazochafua sifa na utu wa wengine. Watawa wajadili na kupata suluhu ya shida na changamoto zao katika vikao maalum, wasiwe ni watu kulalamika daima, bali yote wayafanye kwa sifa na utukufu wa Mungu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa watawa kuratibu vilema vyao na huu utakuwa ni msaada mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kuambata utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anawataka watawa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini na kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa na idadi ya watawa wanaoingia kila mwaka kiasi cha kuyafanya maisha ya kitawa kuwa kama nyumba ya wagumba! Mwelekeo kama huu ni hatari kwani kuna kishawishi kikubwa cha kutaka kuwakusanya wote, wanaofaa na wasiofaa katika maisha na utume wa Kanisa kama watawa. Waombaji wa maisha ya kitawa wanapawa kuchaguliwa kwa umakini mkubwa, kusaidiwa katika malezi na majiundo awali na endelevu, kwa kuwa na matumaini daima. Watawa wasali na kutafakari zaidi Neno la Mungu, sanjari na kutolea ushuhuda wa maisha ya kitawa yenye mvuto na mashiko.

Watawa wasali zaidi ili kumwomba Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi ambao ni wachapakazi, wema na watakatifu. Watawa wasipohamasisha miito mitakatifu, watajikuta wanamezwa na malimwengu kwa kupenda kukumbatia fedha na hapo ndipo kuna kilio na kusaga meno anasema Baba Mtakatifu. Watawa wanaingia katika hofu ya uzee na matokeo yake ni ubinafsi na uchoyo. Matumaini ni chemchemi inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, fedha ni fedheha na imekuwa ni anguko la watawa wengi katika maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza watawa kwa kujisadaka bila kujibakiza kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa. Hawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaojionesha katika sekta ya afya, elimu na maendeleo endelevu ya mtu kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawashukuru watawa wanaoendelea kujisaka sehemu mbali mbali za dunia, watawa ambao waliyamimina maisha yao wakiwa vijana wadogo kabisa, ushuhuda unaojionesha kwenye makaburi ya wamissionari sehemu mbali mbali za dunia.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume kwa mikakati yote waliyoipanga na kuitekeleza kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Amekazia unabii unaojikita katika utii, ujirani mwema kama sehemu ya mchakato wa ushuhuda na matumaini kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, chanzo cha miito mitakatifu ndani ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.