2016-02-02 08:11:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Uongozi, Malezi, Rasilimali fedha na Uinjilishaji!


Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume akimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na zaidi ya watawa 5, 000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama tukio la kuhitimisha maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Jumatatu tarehe Mosi Februari 2016 amesema, hili ni tukio muhimu kati ya matukio makuu matatu ambayo yamefanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yaliyojikita katika majadiliano ya kiekumene, malezi na utume kwa vijana.

Kongamano la Watawa Kimataifa kwa mwaka huu, limewakusanya watawa wa mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume pamoja na yale ambayo yameanzishwa hivi karibuni baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Tukio hili limekuwa ni baraka kwa watawa kukutana na kuzungumza pia na Baba Mtakatifu Francisko. Kongamano hili limekuwa ni kipindi cha kuadhimisha, kusali, kutafakari na kushirikisha mang’amuzi kuhusu maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa bila kusahau changamoto na makwazo wanayokutana nayo kila siku ya maisha yao. Watawa wamejenga na kudumisha umoja na udugu.

Kardinali Braz de Aviz amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, wamefakari kwa kina changamoto aliyowapatia kwa kuwataka watawa kuwaamsha walimwengu; kuwa mabingwa na wataalam wa ujenzi wa umoja, tayari kutoka kimasomaso ili kuwashirikisha watu wa mataifa, mambo msingi katika maisha yao, ili kuonja thamani, utu na heshima ya binadamu, hususan maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa wanapaswa kuwa na jicho la huruma kwa wakimbizi na wahamiaji, wagonjwa na wazee bila kuwasahau vijana wanaojikatia tamaa ya maisha. Watawa wawe ni alama ya matumaini kwa kujibu kilio cha watu mbali mbali!

Watawa wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaonesha dira na mwelekeo sahihi ya maisha na utume wa kitawa. Kanisa linatambua kwamba, kuna idadi kubwa ya watawa wanaolegea na hatimaye kushindwa kuendelea na maisha na utume wao kama watawa pamoja na kuchechemea kwa miito ndani ya Kanisa katika maeneo mengi. Bado kuna changamoto kubwa ya kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kijumuiya katika upendo na udugu! Zote hizi ni changamoto ambazo zimekuwa ni chachu ya imani na matumaini mapya, tayari kuanza mchakato wa kujikita katika njia inayowapeleka watawa katika umoja na udugu; malezi na majiundo endelevu; kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma ya mapendo pamoja na kutumia vyema rasilimali vitu na fedha kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji mpya. Changamoto zote hizi zinahitaji toba na wongofu wa ndani ili kuambata njia mpya ya mageuzi ndani ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.