2016-02-01 10:53:00

Wosia wa Papa Francisko kwa watawa: Unabii, Ujirani na Matumaini!


Yesu kwa njia ya huruma na upendo wake usiokuwa na kifani anamwita mtawa na kuitikia mimi hapa tayari kumfuasa Kristo Yesu. Wakati mwingine wito huu unajibiwa kwa furaha na bashasha, wakati mwingine kwa mateso na wasi wasi mkuu; kwa kuonesha ukarimu na kufuata njia ambayo Yesu mwenyewe amewatayarishia wafuasi wake, ili kukaa pamoja naye; katika utume na huduma; kwa kubeba Msalaba kiasi hata cha kuyamimina maisha. Watawa wamebahatika kupewa karama ya Roho Mtakatifu ili waweze kuwapenda maskini na wadhambi.

Watawa kwa kutembea pamoja na Yesu wamejifunza kutoka kwake jinsi ya kuhudumia na kuonesha ukarimu; kusamehe na kupendana kidugu. Maisha ya wakfu yanapata maana ya pekee kwa kuungana na kushikamana na Kristo Yesu, tayari kutoka kimasomaso kumpeleka katika viunga na maisha ya watu, kwa kumuiga, kwani Kristo anawaunda na kuwa Kanisa, zawadi kwa binadamu!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe Mosi Februari 2015 wakati alipokutana na watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Watawa Duniani sanjari na hitimisho la Mwaka wa Watawa Duniani ambao umelisaidia Kanisa kuonesha mn’gao wa uzuri na utakatifu wa maisha ya kitawa; majitoleo na furaha ya majibu ya wito wao kwa Kristo. Watawa wameng’amua kwa uwazi zaidi utambulisho wao, tayari kusonga mbele huku wakiwa wamejikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha, ili kuandika kurasa safi zinazofuata nyayo za waanzilishi wa mashirika yao.

Baba Mtakatifu anamshukuru kwa namna ya pekee Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake wakati wote wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Amelishukuru Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa matayarisho na maadhimisho ya matukio mbali mbali ya Mwaka wa Watawa ndani na nje ya Roma. Hii ni changamoto ya kuendelea kuwa waminifu kwa wito na maisha ya kitawa; kukua na kukomaa katika upendo; sadaka na ugunduzi. Kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu anataka kuwaachia watawa zawadi ya maneno matatu muhimu: Unabii, Ujirani na Matumaini.

Baba Mtakatifu anasema Unabii ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa watawa. Anawataka watawa kushuhudia ukweli wa Kimungu kwa njia ya maisha yao yanayoonesha mng’ao wa sura ya Mungu Baba mwingi wa huruma na mapendo na wala si mwepesi wa hasira. Ikiwa kama watawa watashindwa kukubalika na kupokelewa na watu wanaowahudumia, watambue kwamba, wameonesha sura yao na kuificha Sura ya huruma ya Mungu. Watawa wajenge na kuimarisha mahusiano na urafiki mwema na Mwenyezi Mungu; kwa kumwabudu katika ukimya na sala.

Baba Mtakatifu anawakabidhi watawa Ushuhuda wa ujirani ambao umejidhihirisha kwa namna ya pekee kwa Mungu kujifunua kwa Kristo Yesu, akawa karibu na watu wote, akashiriki furaha na machungu ya watu wake; akabeba mabegani mwake magonjwa na mateso ya mwanadamu, ili kuwa ni fidia kwa wengi. Kumfuasa Kristo ni kujitahidi kufuata nyayo zake kama Msamaria mwema, tayari kuwaganga na kuwaponya waliojeruhiwa; kuwa karibu na watu ili kushiriki furaha na mahangaiko yao, ili kuwaonjesha upendo na sura ya Baba wa milele pamoja na huruma ya Mama Kanisa. Asiwepo mtu anayewaona kuwa ni watu wa kuja! Kila mtawa anaitwa kuhudumia mintarafu karama ya shirika lake: katika sala, katekesi, elimu, afya na matendo ya huruma; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ili kuishi kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu anawahimiza watawa kuwa ni mashuhuda wa Matumaini ya huruma ya upendo wa Mungu, ili kuwaonjesha walimwengu matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu wanaoogelea katika kinzani, woga, wasi wasi na hali ya kukata tamaa. Watawa wawaonjeshe heri za mlimani, uaminifu na huruma; wema, kiasi na kujikita katika mambo msingi na yenye maana katika maisha ya watu. Watawa wawe ni chachu ya matumaini ndani ya Kanisa, kwa kukuza majadiliano ya kiekumene hata na watawa wa Makanisa mengine ya Kikristo. Watawa washuhudie na kumwilisha karama ya mashirika yao katika mitindo mbali mbali ya maisha, huku wakikuza na kudumisha umoja.

Baba Mtakatifu anawataka watawa kuhakikisha kwamba, katika utume wao kamwe wasiongozwe na umri au idadi yao, bali wawe na ujasiri wa kuitikia wito wao kila siku ya maisha, ili kuweza kupyaisha matumaini yao. Unabii, ujirani na matumaini ni mambo yatakayojaza furaha mioyo yao, kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo, mvuto na mashiko kwa watu wengi zaidi kwa ajili ya utukufu wa Mungu na uzuri wa Kanisa, mchumba wa Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.