2016-02-01 08:40:00

Watawa wanapaswa kurejea katika mambo msingi ya maisha na utume wao!


Kardinali Joao Braz de Aviz Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani imekuwa ni fursa kwa watawa kufanya tafakari ya kina kuhusu karama, maisha na utume wao ndani ya Kanisa ili waweze kujikita katika mambo msingi ya maisha. Huu umekuwa ni mwaka wa neema, baraka na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha, wito na utume wa watawa kwa ajili ya huduma kwa Kanisa.

Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanafumbata hazina kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Watawa wapo ingawa hawavumi, lakini wanaendelea kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuonesha utambulisho wao. Mifumo mbali mbali ya maisha ya kitawa, ipo kwa ajili ya kukamilishana! Watawa wa ndani wanajikita zaidi katika sala na tafakari; watawa wa Mashirika ya kazi za kitume, wao wanachakarika katika kuwahudumia watu wa Mungu: kiroho na kimwili katika medani mbali mbali za maisha, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Maadhimisho ya makongamano, sala na tafakari katika kufunga maadhimisho ya Mwaka wa Watawa imekuwa ni fursa kwa watawa kuangalia changamoto na fursa mbali mbali ili kuweza kutembea pamoja, huku wakiwa wameshikamana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kuimarisha umoja wa Kanisa kwa kutumia karama mbali mbali za Mashirika ya Kitawa.

Kardinali Braz de Aviz anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu amekuwa kweli ni chachu muhimu sana ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, wa kutambua kwamba, yeye kimsingi ni mtawa amefafanua utajiri unaofumbatwa katika Mapokeo ya Kanisa pamoja na kuwahamasisha watawa kusoma alama za nyakati ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya furaha na huruma ya Mungu kwa waja wake. Hiki ni kipindi cha kujikita katika mambo msingi ya maisha ya kitawa kwa kuitikia kikamilifu wito kutoka kwa Kristo Yesu, bila kigugumizi wala makunyanzi!

Baba Mtakatifu katika mwaka wa Watawa Duniani amekazia kwa namna ya pekee umoja na mshikamano wa watawa na Makanisa mahalia, kama sehemu ya kumwilisha karama za maisha yao pamoja na umuhimu wa kujenga na kudumisha maisha ya kijumuiya yanayofumbatwa katika umoja na utofauti wa tamaduni, lugha, umri, vionjo na makando kando mbali mbali. Maisha ya pamoja ni mchakato unaowatajirisha watawa, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.

Kwa njia hii, watawa wataweza kuwa kwenu ni watangazaji wa Injili ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Ni wakati muafaka wa kuambata mashauri ya Kiinjili kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kristo na Kanisa lake. Mashauri haya ni zawadi kubwa kutoka kwa Kristo kwa ajili ya Kanisa lake. Ni zawadi zinazokabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu mamboleo, lakini kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu, watawa wanaweza kushinda vikwazo na changamoto zote hizi, wakawa tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, yanahitimishwa wakati Kanisa linaendelea kushika kasi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika maisha na huduma mbali mbali wanazozitoa kama kielelezo cha Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Watawa wana mchango mkubwa katika mchakato wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwani hii ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wao ndani ya jamii. Mtawa asiyekuwa na huruma, huyo ana matatizo katika maisha yake! Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uwe ni mwendelezo wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zilizopewa kipaumbele cha pekee wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Mahitimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni mwanzo mpya wa maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.