2016-02-01 11:56:00

Unyenyekevu ni njia inayompeleka mwamini katika utakatifu wa maisha!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu tarehe Mosi, Februari 2016 amesema, unyenyekevu ni njia inayomwelekeza mwamini katika utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu amegusia unyenyekevu ulioneshwa na Mfalme Daudi, aliyetambua udhaifu wake wa kibinadamu, akakubali kudhalilishwa mbele ya watu kwani alikuwa na imani na matumaini kwa huruma na upendo wa Mungu.

Lakini, Baba Mtakatifu anaonya kwamba, rushwa na ufisadi ni madonda ambayo si rahisi sana kuponyeka kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia. Mfalme Daudi alikuwa ni mdhambi, lakini hakuwa mla rushwa wala fisadi anakubali kwamba alitenda dhambi ya mauaji ya mtu asiyekuwa na hatia na kwa njia hii upanga ukaingia nyumbani mwake.

Mfalme Daudi anapambana na kijana wake Absalomu ambaye amegeuka kuwa fisadi anataka kumwangamiza, anakubali kukimbia mji na kuliacha Sanduku la Agano kwani hakutaka kumtumia Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao yake binafsi. Mfalme Daudi anaamua kuachia ngazi ili kuwaokoa watu wake anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Daudi analia na kumwomba Mungu toba, anakubali matusi na laana ya Shimei kwa kuamini kwamba, hii ni laana kutoka kwa Mungu.

Daudi alibahatika kusoma alama za nyakati, anakubali kunyenyekeshwa kama sehemu ya toba kutokana na dhambi zake na baadaye anajiaminisha kwa Mungu, njia inayomkirimia utakatifu wa maisha. Waamini wajifunze kutafakari hija ya maisha yao, wasiwe wepesi kutoa majibu ya haraka haraka wala kutaka kulipiza kisasi. Wakristo wawe na ujasiri wa kuomba neema ya unyenyekevu kwa kukubali kudharauliwa, ili kufikia hatima ya utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ambao Mwenyezi Mungu anawakirimia watu wake analikirimia Kanisa pia kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Mwanaye Mpendwa Yesu, ili kuwaonesha waja wake njia inayowapeleka kwenye utakatifu wa maisha. Mfalme Daudi kwa kukubali kunyenyekeshwa na kudharirishwa alikua anamtabiria mateso hayo Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mungu neema ya unyenyekevu ili waweze kufikia utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.