2016-02-01 14:45:00

Manabii wanatumwa kutangaza na kushuhudia Ukweli wa Neno la Mungu


Mhubiri maarufu Padre Munachi anasimulia kisa cha askofu mmoja mzalendo huko Nigeria ambaye baada ya kupata daraja la uaskofu, anarudi katika jimbo lake na kupata mapokezi makubwa. Watu wale walikuwa na imani ya kawaida tu na hata pengine hawakujua vizuri cheo cha Askofu. Wengi walimpongeza kama mtu ambaye tayari njia yake ya mbinguni iko wazi. Wakamwahidi kuwa wangekuwa wote wakristo kama angeondoa amri moja katika amri kumi. Kabla hawajasema ni amri ipi, askofu akawakumbusha kuwa amri za Mungu haziwezi kuguswa na mwanadamu. Hapa sherehe yote ikaharibika. Ilibidi Askofu aondoke haraka katika mazingira yale kwani hali ilikuwa mbaya kabisa. Hiki ndicho kilichompata Yesu pia katika Injili ya leo.

Kama yule Askofu, hapa tunaona Yesu anarudi nyumbani mara baada ya ubatizo wake ambapo Roho Mtakatifu anashuka juu yake na anatangazwa kuwa mwana mpendevu wa Mungu. Na watu wake walimpokea kwa shangwe. Wote waliongea vizuri juu yake. Ugomvi ulitokea pale ambapo Yesu aliongea ukweli juu ya mapenzi ya Mungu. Yeye alikuwa nabii, Yule ambaye anaongea mahali pa Mungu, msemaji wa Mungu. Alama ya unabii ni hii ‘hivi ndivyo asemavyo Mungu’. Nabii huongea Neno la Mungu iwe linafaa au halifai.

Nabii husema ukweli mchungu, na hapa ndo ugomvi huanza. Somo la Injili laonesha wazi hali hiyo. Ukweli anaosema Yesu upo katika Injili ya leo kulikuwa na wajane wengi …. Wao waliamini Mungu ambaye walimtengeneza wao. Walibinafsisha mapenzi ya Mungu na kujiona kuwa wao ndio wateule tu na wengine hawawezi kupata nafasi hii. Hivyo hawakuwa tayari kupokea ukweli mwingine.

Katika somo la kwanza twaona habari juu ya ufunuo wa upendo mkuu wa Mungu – kabla siakuumba nilikujua na kabla hujzaliwa nalikutakasa – nabii alitengwa kwa ajili ya Mungu. Sisi katika ubatizo ni kama nabii – kumwabudu Mungu, kutii amri zake, kutangaza Neno lake, kutumikiana na kupendana. Wito wetu ni kuwa tayari – 1Fal. 18:46, Ayu. 38:3; 40:7, Mt. 25:13. Hakuna ajuaye kitakachotokea kwanza – kama Bwna Yesu atarudi na utukufu na malaika wake mwisho wa nyakati au kama tutaitwa mbele ya kiti cha haki mwisho wa maisha ya hapa duniania. Mt. Pt. 1Pt. 5:6-10 anatoa jibu – basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari … muwe na kiasi, kesheni n.k

Katika somo la pili – Wakorintho wanashindana ni zawadi ipi ni kubwa zaida – kuongea kwa lugha, unabii, ufahamu wa fumbo la Mungu au imani. Mt. Paulo anasema ni upendo. Ule upendo utokao kwa Mungu kwa njia ya Kristo. Upendo usio na mipaka – Agape – upendo utokao kwa Mungu Baba kwa njia ya mwanae.  Sababu ya ukuu wa upendo ni kwamba watoka kwa Mungu. Vipaji vya Roho Mtakatifu vina ukomo, isipokuwa upendo. Sababu Mungu ni upendo – 1Yoh. 4:8 na kwamba upendo watoka wa Mungu – 1Yoh. 4:7 na wote wampendao wabaki kwake – 1Yoh. 3:24.

Pengine hatuoni kitu cha pekee sana, yaani kama changamoto kutoka masomo yetu ya leo. Kikubwa tulichona ni ule utayari wa kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Tumeona katika maisha ya Yesu, ya nabii Yeremia na katika somo la pili. Je ni kwa namna gani tunaweza kufananisha maisha yetu na na maisha yao? Kwamba ‘hvi ndivyo asemavyo Mungu? Na kusema tu Neno la Mungu hata kama litagharimu maisha yetu? Tukifanya hivyo tutakuwa tumetimiza mapenzi yake Mungu na kuwa manabii wake katika ulimwengu wetuwa leo.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.