2016-02-01 09:38:00

Hatima ya maisha ya kitawa ndani ya Kanisa!


Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, kongamano la kimataifa kama sehemu ya mchakato wa kufunga maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani  kuanzia tarehe 28 Januari  2016 imekuwa ni fursa makini ya kuangalia maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa kwa jicho la kinabii, ili kufanya tafakari ya kina, kuhusu uwezo na mapungufu ya watawa katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazowasibu watawa. Lengo ni kuangalia hatima ya maisha ya kitawa kwa siku za usoni!

Askofu mkuu Carballo anakaza kusema, watawa wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwenye Makanisa mahalia. Watawa wagundue ndani mwao, ule upendo waliokuwa nao siku ile walipoitikia kwa mara kwanza wito wa maisha ya kitawa na kazi za kitume, tayari kusoma alama za nyakati, ili kujibu kilio na matarajio ya watu wa nyakati hizi. Taasisi na utume unaotekelezwa na watawa katika medani mbali mbali za maisha ni muhimu!

Lakini, Kardinali Joao Braz de Aviz Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, jambo la muhimu ni watawa kushuhudia uwakfu wao unaobubujika kutoka kwenye Sakramenti ya Ubatizo katika maisha na huduma wanayoitoa kwa watu mbali mbali. Lengo ni kukuza dhana ya ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano. Mashauri ya kiinjili ni ushuhuda wa uhuru pasi na shuruti, zawadi ya Kristo kwa Kanisa lake; zawadi inayopaswa kulinda na kuendelezwa kwa uaminifu na ujasiri.

Askofu mkuu Carballo anafafanua kwamba, mifumo mbali mbali ya maisha ya kitawa ndani ya Kanisa ni kielelezo cha ufahamu wa Kanisa unaojikita katika umoja kwani karama zote ni mashirika ya kitawa ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa. Karama zinatofautiana na kukamilisha katika maisha na utume wa Kanisa. Karama zote ni nzuri na muhimu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu.

Sr. Nicla Spezzati, ASC, Katibu mkuu msaidizi Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, watawa wanaogopa changamani za nyakati hizi. Lakini wanapaswa kukumbuka kwamba, hiki ni kipindi cha neema, Mwenyezi Mungu anaendelea kutenda kazi kati ya watu wake. Hizi ni nyakati changamani na zenye changamoto nyingi, licha ya magumu yote, lakini watu bado wana uwezo wa kupanga na kutekeleza sera na mikakati yao kwa njia ya umoja na mshikamano. Huu si muda wa kuishi katika upweke hasi, kwani huko watawa wanaweza kuteseka sana!

Watawa wanapaswa kuhakikisha kwamba, tasaufi yao inamwilishwa katika uhalisia wa: historia, nyakati na maisha ya watu. Watawa wafahamu, wajitahidi kuiishi na kutafakari tasaufi yao. Siku ya Jumapili, watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia walipata nafasi ya kutembelea Makanisa makuu yaliyoko mjini Roma na kusali ndani ya Makanisa haya kama nafasi ya kuadhimisha pia Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Watawa wamepembua na kutafakari kwa kina kuhusu umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; maisha na utume wa vijana; mawasiliano na dhana ya utamadunisho. Hatima ya maisha na utume wa watawa kwa siku za usoni unajikita katika hija ya pamoja; malezi makini pamoja na kupanga na kuteleleza sera na mikakati ya maisha na utume wa Kanisa katika umoja na udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.