2016-01-31 14:06:00

Mshikamano wa upendo na udugu na wagonjwa wa Ukoma!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 31 januari 2016 amegusia Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa wa Ukoma Duniani, ingawa unaendelea kudhibitiwa sehemu mbali mbali za dunia, lakini bado una madhara makubwa kwa watu, hasa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapa kuna haja ya kuendeleza mshikamano wa upendo na wagonjwa wa Ukoma. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia sala na baraka zake wale wote wanaowahudumia wagonjwa wa Ukoma.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya siku ya 73 ya Wagonjwa wa Ukoma Duniani, kuonesha mshikamano wa pekee, ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya wagonjwa hao. Ni wakati wa kuonjesha huruma ya Mungu, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baraza la Kipapa linaendelea kujipanga vyema katika maadhimisho ya mshikamano na wagonjwa wa Ukoma, kwa semina ya siku mbili kuanzia tarehe 10-11 Juni 2016 na kuhitimishwa na Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wagonjwa na walemavu. Huu ni mkakati wa kukoleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani; kwa kutoa habari sahihi, ili kukinga na kuponya, pamoja na kuwawezesha wagonjwa waliopona kuweza kurejea tena ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana alikuwa na wawakilishi wawili wa Chama cha Vijana Wakatoliki Jimbo kuu la Roma, ambao walikuwa wamesindikizwa na wazazi pamoja na walezi wao baada ya kufanya “Maandamano ya Amani” huku wakiwa wanataka kuonesha ushuhuda wa amani inayorutubishwa kwa imani kwa Kristo Yesu. Vijana hawa wamepita katika Lango la Huruma ya Mungu kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Vijana wamesoma risala ya amani na matumaini kwa dunia bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.