2016-01-31 11:23:00

Kongamano la Ekaristi Takatifu, Cebu, moto wa kuotea mbali!


Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa linaloongozwa na kauli mbiu“Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu” na kuadhimishwa Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini, ni tukio linaloonesha umoja, upendo, mshikamano, ukarimu na imani ya Kanisa Katoliki katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Wajumbe 15, 000 kutoka katika nchi 70 wameshuhudia, wameguswa, wametafakari na kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, shule ya umoja, huduma, upendo na huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wawezeshaji wa Kongamano hili wamegusia umuhimu wa Ekaristi Takatifu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa kama kielelezo cha kumwilisha Imani ya Kanisa kuhusu Ekaristi Takatifu katika uhalisia wa maisha ya watu, kwani Ekaristi Takatifu ni chachu ya mageuzi yanayojikita katika haki, amani, upendo na mshikamano, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza, kwani huyu ndiye sababu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa wafu. Wakatoliki wameonesha imani yao kwa Yesu wa Ekaristi Takatifu kwa kushiriki katika maandamano yanayoshuhudia uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake.

Takwimu zinazonesha kwamba, waamini zaidi ya millini moja na nusu wameshiriki katika Maandamano ya Ekaristi Takatifu Jimbo kuu la Cebu, kama sehemu ya maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Watoto 5, 000 wamepokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza katika maisha, tayari kuwa kweli ni mashuhuda wa upendo wa Mungu kwa watoto wenzao nchini Ufilippini. Wachunguzi wa mambo wanasema, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu huko Cebu, Ufilippini imekuwa ni sherehe ya kukata na shoka! Watu wametafakari, wamesali, wameandamana na kushuhudia imani yao kwa Yesu wa Ekaristi, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, changamoto ya kujenga na kudumisha moyo wa upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, katika tafakari yake amewataka waamini kuondokana na utandawazi usioguswa wala kujali mahangaiko ya jirani zao, bali wawe tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia matendo ya huruma kiroho na kimwili, yakimwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kardinali Tagle amefafanua kwa kina na mapana kuhusu Ekaristi takatifu na majadiliano na tamaduni za watu. Anasema, ulimwengu mamboleo unapenda kujipambanua kwa kuwa na ufanisi, utajiri na maisha bora zaidi, hata kama si mambo msingi katika maisha. 

Uchoyo na ubinafsi ni jamvi la rushwa na ufisadi, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati ili kukoleza mafungamano ya kijami, mwelekeo sahihi wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ekaristi Takatifu ni shule ya huduma, upendo na mshikamano wa kweli kati ya watu, tayari kuambata msingi ya haki, amani na upatanisho.

Kardinali Gaudencio B. Rosales, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini amewatafakarisha wajumbe kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu na Utume wa Kanisa, kama mwendelezo wa Amri ya Kristo “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”. Kila wakati waamini wanaposhiriki kwa ukamilifu wakiwa katika hali ya neema wanampokea Kristo, ambaye anakuwa ni sehemu ya maisha yao; chachu ya mabadiliko na changamoto ya ushuhuda wa upendo katika medani mbali mbali za maisha.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya Ekaristi na utume wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo wa Kristo kati ya watu wa mataifa. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni mahali pa kuendeleza huduma ya Kikuhani, kwa Wakristo kutambua kwamba, kwa njia ya Ubatizo, wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria amefafanua kwa kina na mapana kuhusu Ekaristi kama jukwaa la majadiliano na maskini pamoja na wote wanaotseka: kiroho na kimwili. Hapa waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanapokea Ekaristi Takatifu si kwa mazoea, bali wakiwa katika hali ya neema, ili kweli Kristo aweze kuwapatia nguvu na hamasa ya kushuhudia imani yao inayomwilishwa katika matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji.

 

Kardinali Timothy Dolan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la New York Marekani, amewashukuru na kuwapongeza Wakleri kutoka Ufilippini ambao wamekuwa wamissionari na wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo nchini Marekani na Barani Ulaya. Wakleri hawa wamekuwa ni msaada mkubwa kwa Kanisa katika maeneo haya kutokana na ukosefu wa wakleri. Waamini kutokana Ufilippini ni wakarimu kwa asili na mashuhuda wa imani na utamaduni wao unaojikita katika misingi ya Kiinjili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.