2016-01-29 07:26:00

Waonjesheni wagonjwa: huruma, upendo na ujirani mwema!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la wafanyakazi katika sekta ya afya akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican Alhamisi tarehe 28 Januari 2016 amegusia kuhusu maadhimisho ya Siku ya XXIV ya Wagonjwa Duniani itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 6 Februari na kufikia kilele chake hapo tarehe 13 Februari 2016 mjini Nazareti. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kujiaminisha kwa Yesu mwenyehuruma kama Bikira Maria. Lolote atakalowaambia, fanyeni” Yoh. 2:5.

Askofu mkuu Zimowski katika hotuba yake amekazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani ambayo kwa mwaka huu yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambamo wafanyakazi wa sekta ya afya wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa wagonjwa. Jumuiya za Kikristo zinaalikwa kujenga na kudumisha ujirani mwema na wagonjwa ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Askofu mkuu Zimowski anasema, maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2016 ni mwaliko kwa familia ya Mungu kutafakari kwa mara nyingine tena muujiza wa kwanza uliotekelezwa na Yesu pale mjini Kana ya Galilaya, alipogeuza maji kuwa divai na hivyo kuwarudishia tena wanaarusi ile furaha iliyokuwa inaanza kutoweka kama umande wa asubuhi. Huu ni muujiza ambayo ulifanywa na Yesu kwa ombi maalum kutoka kwa Bikira Maria.

Maadhimisho haya yanafanyika mjini Nazareti, mahali ambapo Neno wa Mungu alitwaa mwili na kukaa kati ya watu wake. Hapa ni mahali alipoanzia utume wake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, tayari kumwonjesha huruma na upendo wa Mungu. Yesu katika maisha na utume wake, aliweza kuwaponya wagonjwa wengi sanjari na kuwaondolea dhambi zao. Mara kwa mara watu walikimbiloia huruma ya Yesu kwa ajili ya wagonjwa na ndugu zao waliokuwa kufani. Matukio yote haya yanaipamba Habari Njema ya Wokovu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, hata wao kwa nyakati hizi wanaalikwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa kuwa na imani thabiti kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hata leo hii kuna watu wengi wanaoendelea kuteseka kiroho na kimwili, wote hawa wanahitaji kuonjeshwa huruma ya Kristo hata kama wanatambua kwamba, si kila mgonjwa anaweza kupona, lakini hapa jambo la msingi ni kuwa na imani thabiti, tayari kumwendea Yesu mganga mkuu wa maisha ya binadamu: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Zimowski anawahamasisha waamini kuwa karibu na wagonjwa, ili kuwaonjesha ule moyo wa ubinadamu unaosheheni huruma, upendo na mshikamano. Dhamana hii inaweza kutekelezwa vyema zaidi na wafanyakazi katika sekta ya afya na taasisi zote ambazo zimepewa dhamana ya kusimama kidete ili kuendeleza afya ya binadamu. Hizi ni hospitali, nyumba za wazee, walemavu na watoto yatima. Huduma kwa wagonjwa ni kipimo muhimu sana kinachoonesha jinsi ambavyo jamii inajali Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kwa upande wake, Monsinyo Jean-Marie Mate Musivi Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi wa sekta ya afya amechambua historia ya maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II na kwa mara ya kwanza siku hii ikaadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa hapo tarehe 11 Februari 1993. Tangu wakati huo, hii ikawa ni Siku ya Wagonjwa Duniani.

Monsinyo Mupendawatu anakaza kusema, kuna tofauti kubwa kati ya Siku ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa na Siku ya Afya Duniani, inayoadhimishwa na Shirika la Afya Duniani, WHO. Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa upande wa Kanisa ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hapa Kanisa linapenda kujikita katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya kudumisha Injili ya uhai. Hapa mgonjwa anapewa kipaumbele cha kwanza ili aweze kupatiwa tiba muafaka.

Padre Augusto Chendi, Katibu mkuu msaidizi kwa upande wake, amepembua umuhimu wa siku hii mintarafu taalimungu ya shughuli za kichungaji na umuhimu wa waamini kutoa ushuhuda kwa kuwatembelea wagonjwa katika maeneo mbali mbali ya Makanisa mahalia kama sehemu ya maadhimisho haya. Kwa njia hii, waamini watakuwa wanamwilisha upendo na huruma kama alivyoonesha Bikira Maria kwa wanaarusi wa Kana ya Galilaya. Wagonjwa waoneshwe na kuonjeswa huruma na upendo wa Mungu.

Maadhimisho kwa Mwaka huu, yatakwenda sanjari na kongamano la afya litakaloadhimishwa huko Notre Dame, hapo tarehe 9 Februari 2016. Hii itakuwa ni fursa ya kuangalia kwa kina na mapana: matatizo, fursa na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya afya, ili kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Kuna haja ya kuwa na mwelekeo wa huruma na mapendo kwa wagonjwa walioko kufani, kwa kuwapokea na kuwahudumia kwa upendo.

Hii ni mada inayopaswa kufanyiwa kazi na kamati za maadili kwa Makanisa mahalia, ili kuhakikisha kwamba, binadamu anapewa kipaumbele cha kwanza katika huduma za afya na kwa namna ya pekee huko Nchi Takatifu. Haya ni matumaini yaliyoonesha na Padre Chendi sanjari na majiundo makini kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Sera na mikakati ya maboresho ya huduma ya afya isimamiwe barabara kwa kuvihusisha vyombo vya sheria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.