2016-01-29 13:40:00

Wanasiasa msichochee vurugu Zanzibar, damu ya watanzania itawalilia sana!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim M. Majaliwa,amesema serikali imeweka msisitizo katika kuhakikisha inarudisha nidhamu kwa watumishi wa umma kwa kuweka mkazo katika uadilifu, uwajibikaji, kutoa huduma kwa wakati. Waziri mkuu Majaliwa ameyasema hayo katika mkutano wa pili kikao cha tatu Bungeni Mjini Dodoma alipokua akihitimisha hoja ya kujadili hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa siku ya ufunguzi wa Bunge la kumi na moja tarehe 20 Novemba 2015.

Amesema kuwa serikali itakuwa inawakumbusha watanzania na watendaji wa serikali kufanya majukumu yao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za haraka dhidi ya watumishi wanaokwenda kinyume na misingi ya utendaji kazi serikali kwa kuzingatia kauli mbiu ya hapa kazi tuu. Pia amesema kuwa baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge ambazo utekelezaji wake utahitaji kutengewa fedha za uandalizi wa kutenga fedha za serikali na utendaji wake utafanyika kwa haraka kwa kuzingatia maombi na hoja za wabunge kwa kusimamia mapato ya Taifa ili yaongezeke kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa mapato ya ndani ya kodi na ambayo siyo kodi ni lazima yakusanywe kikamilifu kwa mujibu wa sheria bila upendeleo na kuwaonea huruma wakwepa kodi nchini. Mhe. Mpango ameyasema hayo kwenye mkutano wa pili kikao cha tatu Bungeni Mjini Dodoma alipokua akijibu hoja mbalimbali za wabunge walizochangia na kujadili hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa siku ya ufunguzi wa Bunge la kumi na moja tarehe 20 Novemba 2015. Dkt. Philip Mpango amesema ni lazima watumishi na walipa kodi kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kupata fedha ambazo zitawasaidia wananchi wa vijijini kupata maendeleo kwa kupata huduma bora na muhimu.

Wakati Bunge likieleza kuwa haliwezi kuzuia vituo vya televisheni nchini kuonyesha moja kwa moja matangazo ya shughuli za vikao vya Bunge, Serikali imetoa sababu tatu za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupunguza matangazo hayo ya shughuli za chombo hicho chenye mamlaka ya kutunga sheria. Uamuzi wa Serikali kuhusu TBC ulizua “sintofahamu” bungeni na kusababisha Polisi kutumika kuwatoa katika Ukumbi wa Bunge, wabunge wa upinzani waliokuwa wakishinikiza kusitishwa kwa mjadala wa hotuba ya Rais John Magufuli, badala yake lijadiliwe suala hilo la shirika hilo.

Naibu Katibu wa Bunge, John Joel alisema kuwa hakuna televisheni yenye mkataba na Bunge kurusha moja kwa moja matangazo hayo, zote zinazorusha zinatumia gharama zao wenyewe. Baada ya TBC kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge, televisheni zilizobaki ambazo zinarusha moja kwa moja matangazo hayo, ni Star TV kupitia chaneli yake ya Star Bunge pamoja na Azam TV. “Sisi hatuna mkataba nao, wao wanarusha kwa gharama zao na Bunge haliwezi kuwazuia, labda waulizwe wenyewe kama wataendelea kurusha matangazo hayo ama laa,” alisema Joel huku akisisitiza kuwa hakuna zuio lolote.

Waziri wa Habari, Nape Nnauye alizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kueleza sababu tatu za kupunguzwa kwa matangazo hayo. Nape aliitaja sababu ya kwanza kuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji, “Kwa mwaka TBC ilikuwa inatumia Sh 4.2 bilioni kurusha moja kwa moja matangazo haya. Fedha hizi hazilipwi na Bunge wala Serikali, zinatokana na matangazo madogo ya TBC, sasa pia hesabu tangu 2005 mpaka sasa zimetumika kiasi gasi.”

Alisema sababu nyingine ya kupunguza kurushwa kwa Bunge ni kutaka wafanyakazi wa Serikali kufanya kazi kikamilifu, kwa madai kuwa wengi badala ya kufanya kazi walikuwa wakifuatilia vipindi hivyo. Alisema utafiti uliofanywa na Serikali umebaini kuwa waendesha bodaboda, mamalishe, wamachinga, wakulima, wafugaji na watu wenye shughuli nyingi wanashindwa kufuatilia vipindi vya Bunge asubuhi na mchana kutokana na kubanwa na shughuli zao.

Kuhusu sakata la Uchaguzi Zanzibar Serikali imesema uamuzi wa kurudia uchaguzi wa Urais Zanzibar ni halali na wa kisheria na kwamba wanaotafuta suluhu nje ya Katiba, wanakosea. Kauli hiyo ilitolewa mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba alipokuwa akihitimisha majadiliano ya kuchangia hotuba ya Rais John Magufuli. Alisema uchaguzi ulifutwa kisheria na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa Tangazo la Serikali Namba 6587. Makamba alisema Katiba ya Zanzibar, imeeleza wazi kuwa hakuna mamlaka ambayo itahoji uamuzi wa tume, hata kama ni Mahakama. Alisema akidi ilitimia wakati tume inafikia hatua hiyo.

Waziri huyo alisema wanaotaka kutumia suala hilo kuleta vurugu Zanzibar, damu ya Watanzania itawalilia. Alisema viongozi wakuu wa nchi, wamefanya kazi kubwa katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo na hivyo ieleweke kuwa ZEC na NEC ni tume zinazojitegemea. Alisisitiza NEC haiwezi kuingilia uamuzi wa ZEC, kwani uchaguzi wa Rais uliofanyika kwa siku moja Tanzania Bara na Zanzibar, umekuwa ukiendeshwa na Tume mbili tofauti. Alisema uchaguzi huo, ulifanywa na tume tofauti na hata wino uliotumika katika chaguzi hizo ni tofauti .

Alisema wajibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuhakikisha kuwa amani na utulivu, vinalindwa Zanzibar katika marudio ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu. Oktoba 28 mwaka 2015, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”. Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”.

Na mwandishi maalum kutoka Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.