2016-01-29 08:37:00

Jimbo kuu la Nairobi, kumekucha! Hitimisho la Mwaka wa Watawa Duniani!


Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yalitishwa na Baba Mtakatifu Francisko yalilenga kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Hati kuhusu Mapendo Kamili “Perfect caritatis” na Mwanga wa Mataifa, “Lumen gentium”. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliwataka watawa kupyaisha maisha kwa kusoma  alama za nyakati sanjari na kuendelea kujikita katika Mashauri ya Kiinjili; maisha ya Kijumuiya na malezi makini na endelevu kwa watawa, ili kuwawezesha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani yatafikia kilele chake hapo tarehe 2 Februari 2016, Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997. Hapa watawa wote wanahamasishwa kujitokeza ili kumshuhudia Kristo Mwanga wa Mataifa kwa njia ya maisha na utume wao kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Mwaka wa Watawa Duniani umekuwa ni utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa, tayari kuambata ya mbeleni kwa moyo wa matumaini Zaidi.

Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi anaialika Familia ya Mungu Jimboni humo, kuungana kwa pamoja katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu, Jimbo kuu la Nairobi, Jumamosi, tarehe 30 Januari 2016 ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa; watu ambao wamejisadaka ili kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Watawa wanaendelea kuhudumia na kuinjilisha, kumbe, hii ni changamoto kwa wakristo wote kutambua wito na utume wao ndani ya Kanisa hasa wakati huu Mama Kanisa anapojielekeza zaidi katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kardinali Njue anawaalika waamini kuonesha mshikamano wa dhati kwa maskini kwa kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili. Kwa namna ya pekee mwaka huu, mchango huu unaelekezwa kwa maskini wanaoishi katika Parokia ya Mukuru, Jimbo kuu la Nairobi.

Kwa kufunga Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Jimbo kuu la Nairobi, waamini wanaendelea kuambata mwaliko wa toba, wongofu wa ndani pamoja na hija ya imani inayomwilishwa katika Matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini wahakikishe kwamba, wanajipatia neema na rehema inayotolewa na Mama Kanisa katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na habari zaidi kutoka Nairobi zinabainisha kwamba, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameamrisha kufutwa ile sharia ya mashirika ya kidini yam waka 2015 iliyopigiwa makelele na viongozi mbali mbali wa kidini nchini Kenya na kwamba, Serikali kwa sasa itaendelea kuwasiliana na wadau mbali mbali ili kuangalia namna ya kuiboresha zaidi. Lengo la Serikali ni kuendelea kujikita katika ukweli na uwazi pamoja na majadiliano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kenya.

Rais Kenyatta hivi karibuni alikutana na kuzungumza na viongozi wa kidini nchini Kenya waliosikitishwa na uamuzi wa Mwanasheria mkuu wa Kenya kuratibu shughuli za Mashirika ya kidini nchini Kenya. Viongozi wa kidini wanasema, sheria hii ilikuwa haitekelezeki na kwamba, ingekuwa ni mzigo mkubwa kwa wananchi wa Kenya sanjari na kuhatarisha uhuru wa kidini ambayo ni haki ya raia wote wa Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.