2016-01-28 14:25:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


“Leo hii maneno haya yametimia masikioni mwenu”. Kifungu hiki cha maneno ndicho kinafungua Injili ya Dominika hii ya 4 ya mwaka C wa Kanisa. Kusudi tupate kuelewa vema hatuna budi kurejea katika Injili ya Dominika iliyopita tuliposikia Kristo akiwa katika Sinagogi katika kijiji chake cha Nazareti na alisoma sehemu ya kitabu cha Nabii Isaya ambacho kilikuwa ni maneno ya matumaini kwa mmoja ambaye alikuwa anatafuta auheni katika maisha. Kristo leo anawapatia hawa ndugu zake na pia anatupatia sisi habari njema. Anajifunua kwa watu wake wa Nazareti na kwa njia hiyo anajifunua kwa wanadamu kuwa ujio wake ndiyo utimilifu wa uaguzi huo wa nabii Isaya. Ujio wake hapa ulimwenguni ni mwanzo mpya kwa maisha ya mwanadamu; ukurasa mpya umefunguliwa ambao unamuweka mwanadamu katika hali njema tena.

Katika lugha adhimu ya Kiswahili upo msemo usemao: “Fadhila mfadhilie mbuzi mwanadamu ana maudhi”. Ujumbe huu wa furaha unapokelewa isivyotegemewa. Fadhila hii ya Mungu kwa mwanadamu inapata mwitikio hasi: “wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo”. Wanashindwa kuipokea huruma ya Mungu inayofunuliwa kwao kwa sababu tu ya unasaba wa mjumbe wa Mungu. Wanashindwa kulipokea Neno na kuanza kumshambulia mtoa neno. Hii ni ajabu kabisa kwani hata kama utafanikiwa kumwangamiza anayekupatia ujumbe wowote ule kamwe hautaweza kuifuta kauli yake aliyoitoa, yaani ukweli alioutangaza.

Sauti ya Nabii ni sauti ambayo inatuletea ujumbe wa Neno la Mungu ambalo daima hunuia lililo jema kwa viumbe vyake. Leo hii tutafakari wajibu na hali ya mtoa ujumbe na mpokea ujumbe. Mtoa ujumbe wa Neno la Mungu anapaswa kutambua kuwa anachokitangaza si maneno yake bali ni Neno la Mungu. Ni wazi kwamba mara nyingi hutokea ukinzani lakini kamwe hali hii isituyumbishe bali tusisitize lile tu lililo Neno la Mungu kama anavyojinasibu mtunga Zaburi akisema: “Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako”. Nabii Yeremia anatuambia katika somo la kwanza kwamba, “usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao”. Hivyo uiamara katika imani na kumtegemea Mungu ndiyo nguzo ya kwanza kwa mtoa ujumbe wa Neno la Mungu.

Jambo la pili analosisitiziwa mtoa Neno la Mungu ni kudumu katika kuitangaza huruma na upendo wa Mungu. Kwa namna ya pekee hapa Mtume Paulo anatueleza katika somo la pili kwamba yote tuyafanyayo kama si katika  upendo yanabaki kuwa si kitu. Hii ina maana kwamba sauti ya kinabii inapaswa kuonjwa kwa namna ya pekee katika upendo wa kimungu unaodumu katika matendo yetu ya kila siku kwa wenzetu. Kamwe tusichotwe na maelekeo ya kidunia ambayo yanaweza kutulaghai na kuona tunahudumia wengine lakini si katika upendo bali kwa ajili ya kutimiza wajibu tu. Upendo wa kimungu unatusukuma na kutufanya kuwa tayari kuifunua nafsi yetu kwa mwingine na kuiona nafsi yake yenye uhitaji wa aina moja au nyingine. Kwa maneno mengine, katika upendo wa kimungu nafsi huongea na nafsi nyingine na hapo kwa hakika Mungu anadumu.

Wapokeaji wa ujumbe wa Neno la Mungu leo wanaonywa kulipokea Neno na kuikwepa ile hali ya kumtathimini anayetoa ujumbe huo. Kama moto unawaka nje ya nyumba yako na kisha akafika mmoja ambaye hupendi kumsikiliza na kukutahadahrisha juu ya balaa hilo, dharau yako juu yake haitabadili ukweli huo kwamba moto unawaka nje ya nyumba yako. Ujumbe wa Mungu ni ukweli na utadumu milele. Tunapoanza kutathimini unasaba, elimu, cheo au hali yoyote ile ya anayekupatia ukweli daima tunajiweka katika hali ya hatari. Watu wa kijiji cha Nazareti wanachukizwa na Kristo na wananuia kumwangamiza bila kuzingatia ukweli wa ujumbe aliowapatia. Ukinzani wao huo kamwe haukubadili na hautabadili ukweli wa maneno yale aliyowaambia. Kristo aliifunua hiyo huruma ya Mungu kwa wanadamu ambayo tunaendelea kufaidika nayo hadi leo hii.

Leo hii tunapewa changamoto: kwanza ni kwa namna gani tunabaki waaminifu katika Neno la Mungu na kulitangaza lilivyo na pili ni kwa namna gani tunaupokea ujumbe wa Neno la Mungu. Aghalabu huwa tunavutwa na upepo wa kidunia na kujaribu kupindisha ukweli kadiri ya Neno la Mungu. Hii mara nyingi hutupeleka katika kuijenga jamii inayohangaika, jamii ambayo inashuhudia daima vilio na huzuni za mwanadamu anayeteseka. Tunapopata fursa ya kufumbua midomo yetu ili kurekebisha hali ambayo inaelekea kuiangamiza jamii ya mwanadamu huwa tunanyamaza kimya. Maneno haya, leo hii maandiko haya yametimia masikioni mwenu, huwa ni nadra sana kusikika kwa watu. Katika adhimisho hili la Jubilei maalum ya huruma ya Mungu tutimize wajibu wetu wa kinabii kwa kupaaza sauti zetu kwa kuleta habari njema kwa watu wote bila kujali macho na maneno ya watu.

Kwa upande mwingine pia, leo tujiweke tayari kuupokea ujumbe wa Neno la Mungu. “Usiche mbachao kwa msala upitao”. Ujumbe wa Neno la Mungu hata kama unagusa maslahi yako fulani fulani kwa faida za kidunia na ambazo hupita tu upokelewe sawasawa. Hiyo ndiyo huruma ya Mungu iliyofunuliwa kwako. Tusizipoteze fursa hizi bali tuwe tayari kuyaacha hayo yanayoifunika sauti ya Mungu na yanayonifanya nisiwe chombo cha kueneza upendo wa Mungu kwa wengine. Upendo wa Mungu unatuunganisha sote na kutufanya tuhudumiane kila mmoja kwa nafasi yake, tuthaminiane kila mmoja kwa nafasi yake na kwa hakika kutufanya kundi moja la wana wapendwa wa Mungu.

Tumwombe Mungu katika Dominika hii ya leo neema ya kuwa na ujasiri wa kulipokea na kulitangaza neno lake na pia kudumu katika upendo wake. Adhimisho la mwaka huu la Jubilei maalum ya Huruma ya Mungu litufanye kila mmoja kuyasikia maneno ya Kristo: “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu” na kwa kutimia huko tupate kuupokea wokovu wa Mungu.Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.