2016-01-28 15:00:00

Rais Faure Essoxima Gnassingbè wa Togo akutana na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 28 Januari 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Faure Essoximna Gnassingbè wa Togo ambaye baadaye alikutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekua ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake, wamegusia uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Serikali ya Togo na kwamba, bado kuna haja ya pande hizi mbili kuendelea kuboresha mahusiano haya. Wamejadili pia mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Togo: kiroho na kimwili, hususan katika sekta ya elimu.

Baba Mtakatifu na Rais wa Togo wamepembua kwa kina na mapana baadhi ya changamoto zinazozikabili nchi za Afrika ya Magharibi na Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kukazia umuhimu  wa Bara la Afrika kujikita katika mchakato wa kujenga, kulinda na kudumisha amani na usalama katika Ukanda huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kisswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.