2016-01-27 09:01:00

Yaliyojiri katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani!


Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani imekuwa ni fursa kwa Familia ya Mungu kuandamana ili kuwafahamu zaidi watawa wanaoendelea kushuhudia utajiri wa Injili katika mazingira magumu na hatarishi; katika umaskini na hali ngumu za kiuchumi; katika mahangaiko ya ndani, dhuluma na nyanyaso katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu.

Watawa ni mashuhuda wa Injili, wanaojisadaka ili kuwaendea watu wanaoishi pembezoni mwa jamii ili kuwaonesha utajiri wa Injili ya huruma ya Mungu. Watawa wanaishi na kumwilisha Injili ya imani, matumaini, huruma na mapendo kati ya watu wanaowazunguka, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yamekuwa na mafanikio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hii imekuwa ni hija ya watawa katika maisha na utume wao, ili kuambata neema na huruma ya Mungu inayowawezesha kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa hata kama mbele yao kuna vikwazo na vizingiti kibao! Watawa wamepata nafasi ya kutafakari kuhusu karama na roho ya mashirika yao, tayari kuiendeleza kwa kusoma alama za nyakati.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amewahamasisha watawa kutoka huko kwenye “viota vyao” walikojificha, huku wakiwa na mwelekeo mpya, waweze kuwa tayari kuwaendelea watu walioko pembezoni mwa jamii, ili kuwashirikisha mambo makuu katika maisha yao. Maadhimisho haya imekuwa ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu taalimungu ya maisha ya wakfu, dhamana, wito na wajibu wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Familia ya Mungu imepata nafasi ya pekee kuweza kutafakari kwa kina na mapana tunu msingi za maisha ya kuwekwa wakfu; maisha ya udugu ndani ya jumuiya; utume wa watawa ndani ya Kanisa; ushuhuda wa maisha ya kitawa katika huduma kwa familia ya Mungu hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Imekuwa ni nafasi kwa watawa kufahamu karama za mashirika mbali mbali, tayari kushirikiana katika kutangaza na kushuhudia Huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya huduma makini.

Kwa hakika imekuwa ni nafasi ya kumshukuru Mungu pamoja na kukuza ukarimu na upendo kwa watawa kwani hawa ni kati ya mihimili mikuu ya Uinjilishaji wa kina. Viongozi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume wametembelea sehemu mbali mbali za dunia na kushiriki katika warsha, makongamano na semina za kitaifa na kimataifa. Huko wameshuhudia jinsi ambavyo vijana wanachangamkia maisha ya kitawa, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa kuambata mashauri ya Kiinjili, yaani: Utii, Ufukara na Useja. Baraza la Kipapa pia katika kipindi cha mwaka mzima limekuwa likitoa tafakari za kina kuhusu umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha; Kusoma Maandiko Matakatifu pamoja na Tafakari ya kina.

Kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya Baraza la Kipapa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika kuhamasisha na kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani. Maadhimisho haya pia yamepata mwelekeo wa pekee katika majadiliano ya kiekumene kwa kutambua kwamba, hata Makanisa mengine ya Kikristo kuna watawa wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Watawa wameweza kufanya mkesha wa sala; watawa vijana wakakutana mjini Roma ili kushuhudia ile furaha ya maisha wakfu kwa ajili ya Mungu na jirani.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yamejikita katika Ibada, Tafakari, Maungamo, Mwongozo wa maisha ya kiroho. Kilele cha maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni kuanzia tarehe 28 Januari hadi tarehe 2 Februari, 2016 Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “ Maisha ya wakfu katika umoja”. Hili ni tukio kuu kwa maisha na utume wa watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko ndiye aliitisha Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani; akawasindikiza katika sala na sadaka yake; akawatajirisha kwa njia ya upendo na tafakari za kibaba; akawaonya kwa njia huruma na upendo wa Mungu. Tafakari zake zimekuwa ni utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa watawa sehemu mbali mbali za dunia. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yatakuwa ni chachu ya maendeleo kwa sasa na kwa siku za usoni.

Kwa njia hii, watawa wataendelea kusonga mbele kwa ujasiri ili kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha na utume wao kwa moyo wa ujasiri pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza na kujibu kilio cha familia ya Mungu kwa nyakati hizi, daima wakimwachia Roho Mtakatifu nafasi ya kuwaonesha dira na njia ya kufuata katika maisha na utume wao.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yamekwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kukazia kwa namna ya pekee, ufuasi wa Kristo wenye mashiko na mvuto; unaoshuhudia na kumwilisha huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Watawa wanapaswa kuwa ni kielelezo cha Msamaria mwema anayethubutu kujitoa mhanga ili kuwaganga wale wanaoteseka kiroho na kimwili kwa njia ya huduma, Sakramenti za Kanisa na faraja ya Neno la Mungu linaloshuhudiwa katika matendo ya huurma: kiroho na kimwili. Bila Injili ya huruma ya Mungu, maisha na utume wa watawa ni sawa na “daladala” iliyokatika usukani, haina mwelekeo wana mashiko katika huduma kwa Mungu na jirani.

Kanisa linatambua na kuwathamini watawa wote kutokana na mchangao wao katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha maisha ya sala, tafakari, udugu na umoja; mambo msingi yanayojenga na kuimarisha maisha ya kitawa na kazi za kitume, kwani wote ni ndugu katika Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.