2016-01-27 14:19:00

Wanafunzi wa CUEA watembelea maeneo ya kimissionari Mombasa!


Umoja wa Kanisa Katoliki unaonekana kwenye kazi ya kitume iliyoanzishwa na Yesu Kristo mwenyewe na kusambazwa kote duniani na mitume pamoja na wamissionari waliojitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao. Kuna umuhimu kwa Wakristo wa nyakati hizi kuthamini historia, dhamana na wito wao unaopata chimbuko katika Sakramenti ya Ubatizo. Wakristo wawe na ujasiri wa kuendeleza kazi na utume ulioanzishwa na wamissionari sehemu mbali mbali Barani Afrika. 

Hayo ni maneno ya Padri Joseph Ekomwa, mratibu wa matembezi ya kihistoria yaliyofanywa na wanafunzi na wahadhiri wa kitengo cha Taalilimungu cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na kati (CUEA) kilichoko Nairobi, nchini Kenya. Mratibu wa ziara hiyo ya kihistoria, Padre Joseph Ekomwa, aliyasema hayo  hivi karibuni wakati akiwa mjini Mombasa kuongoza kundi la wanafunzi 37 kutoka CUEA, ili kutembelea maeneo ya kwanza yaliyotumiwa na Wamissionari katika kupandikiza mbegu ya Ukristo Pwani ya Afrika Mashariki. Maeneo hayo ni pamoja na ngome ya “Fort Jesus” iliyoko kisiwani Mombasa ambako wamissionari wa kwanza  kutoka Ureno walifika hapo kunako mwaka 1593.  

Ngome ya “Fort Jesus” ni ishara ya kudumu inayounganisha mchakato wa Uinjilishaji Pwani ya Afrika Mashariki na Wamissionari wa kwanza wa Shirika la kitawa la Waagostino kutoka Ureno. Wamissionari hao wa kwanza, walipata mateso mengi na wengi wao wakapoteza maisha kutokana na magonjwa na hali ngumu ya maisha, lakini damu yao imekuwa ni mbegu ya Ukristo Afrika Mashariki. Ngome ya “Fort Jesus” ni kielelezo cha juhudi za kimissionari ambazo zimezaa matunda ya ukomavu wa dini ya Kikristo kwa nyakati hizi.

Pia walitembelea Mnara waVasco Da Gama  ulioko mjini Malindi na ulijengwa na Baharia mchunguzi Vasco da Gama kunako mwaka 1498 kama ngome yake ya usalama alipokuwa safarini kuelekea Bara Hindi.  Hatimaye, Francisko Xavier aliigeuza ngome hiyo ya Vasco da Gama kuwa Kikanisa baada ya kuadhimisha ibada ya Misa takatifu mahali hapo kunako mwaka 1552.  Kikanisa hicho hadi sasa kiko imara na kinakaribia kuwa na umri wa miaka 517. Matendo makuu ya Mungu.

Padre Joseph Ekomwa amesema kwamba ina tia moyo kwa vijana wanafunzi kuelewa historia na juhudi za wamissionari wa kwanza katika kupanda mbegu ya ukristo Pwani ya Afrika Mashariki. Wanafunzi waliokuwa kwenye ziara hiyo nao wamesema kwamba ziara hiyo imewafikisha kwenye mizizi ya Uinjilishaji Pwani ya Afrika Mashariki na kwamba wamefurahia kutambua ushuhuda wa imani Mungu aliouonyesha kupitia kwa Wamissionari wa Bara Ulaya walioileta imani ya Kikristo Barani Afrika. 

Wanafunzi hao wa CUEA wanasema wamejisikia kuwa wamoja na Kristo na Kanisa lake, aliyewatuma Mitume wa kwanza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, changamoto kwa Wakristo wa nyakati hizi kusimama kidete kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Na Sr. Bridgita Samba Mwawasi.








All the contents on this site are copyrighted ©.