2016-01-27 10:24:00

Mafungo ya kiroho kwa wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano, tarehe 27 Januari 2016 ambayo wakati huu inajikita kwa namna ya pekee katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anawaalika wafanyakazi wote wanaotoa huduma katika Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali duniani, wakati wa Kwaresima, kutenga siku maalum ya kusali, kufunga na kulitafakari Neno la Mungu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawahimiza kutafakari wito na dhamana yao ya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Siku hii maalum imeandaliwa na Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum. Lengo ni kuwawezesha wafanyakazi hawa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa niaba ya Kanisa, ambalo kweli ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa waja wake.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu  wa Cor Unum wakati akiwasilisha Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresma kwa Mwaka 2016 unaongozwa na kauli mbiu “Nataka rehema na wala si sadaka”  (Mt. 9:13) anasema, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha huruma na upendo wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Kumbe, wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada na Vyama vya Kitume kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wanapaswa kuchagua siku ambayo watafunga, watasali na kutafakari dhana ya huruma ya Mungu katika maisha yao, kama sehemu ya kielelezo cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watu wanaowahudumia.

Kila taasisi, chama au kikundi cha huduma, kiangalie siku na kufanya tafakari ya kina kuhusu hali na mazingira wanamotoa huduma kwa Familia ya Mungu. Wafanyakazi hawa kwanza kabisa wanapaswa kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao, ili waweze kuwa wepesi kuwagawia jirani na wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya huduma kwa jamii. Hapa wafanyakazi hawa wanahamasishwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho ambayo katika mazingira yao, inamwilishwa kwenye matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Cor Unum katika maadhimisho haya imeandaa vitini vinavyoweza kuwsaidia wafanyakazi katika Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Vyama vya kitume na vikundi mbali mbali vya misaada kwa maskini na wahitaji zaidi kuangalia katika tovuti yao inayopatikana kwa anuani ifuatayo: www.corumjubileum.va.

Askofu mkuu Dal Toso anakaza kusema, katika Kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka kumi, tangu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipochapisha Waraka wake wa kitume: Mungu ni upendo, Deus Caritas est, kunako tarehe 25 Januari 2006, Cor Unum kati ya tarehe 25-26 Februari, 2016 itaadhimisha Kongamano la Kimataifa kuangalia mchango wa Waraka huu wa Kitume katika huduma kwa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waraka huu umefungua mwelekeo mpya katika kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto inayoendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hapa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu, kwani Kanisa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu.

Baadhi ya wawezeshaji wakuu ni pamoja na Kardinali Gerhard Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Kardinali Louis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Caritas Internationalis. Viongozi hawa wakuu wa Kanisa watapembua kwa kina na mapana taalimungu inayojikita katika Waraka wa kitume: Mungu ni upendo. Cor Unum pia imewaalika Rabbi David Shlomo Rosen, Professa Saeed Ahmed Khan pamoja na Professa fabrice Hadjadj, kuchangia mada hii kadiri ya mitazamo yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.