2016-01-27 12:02:00

Atibua nyongo ya watu; nao wataka kumwonesha cha mtema kuni!


Ndugu zangu “wivu unaua na wala hauna maua!.” Mnakumbuka dominika iliyopita wote tuliupata mwaliko wa kununua bidhaa kwenye Lembuka au soko bila kutumia pesa. Kumbe, leo tutawaona wenzetu wengine waliozoea vya kunyonga, wanadai kwamba ni wao tu ndiyo wanaostahili kupata vya bure na wengine inabidi wagharimie. Madai hayo yaliibuka kanisani, yakapelekea watu kuzozana hadi kutaka kumdhuru aliyeandaa lembuka yenyewe. Hebu tulifuatilie sakata lilivyokuwa na hatima yake.

Yesu yumo bado hekaluni alimozisoma zile aya mbili kutoka chuo cha nabii Isaya zilizosema: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Huu ulikuwa mwaliko wa Lembuka ya bure ya upendo wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kwetu. Baada ya kusoma aya hizo, Yesu akatoa msimamo wake binafsi:“Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu.” Msimamo huo ndiyo uliotibua mambo na kusababisha sintofahamu kati ya wasikilizaji wake, hadi Sinagogini pakageuka kuwa ukumbi wa mjadala na malumbano.

Vituko hivi vilitokea nyumbani kwake Yesu huko kijijini Nazareti alikolelewa. Yesu anapotumia neno kijiji anamaanisha wenyeji wenye fikra finyu zilizojikita kwenye mila na utamaduni wa kijiji, na hawako tayari kupokea mawazo mapya. Ndiyo maana, kila mara Yesu anapotaka kumponya mtu, kama vile yule kipofu wa Bethsaida anamwongoza nje ya kijiji na baada ya uponyaji huo anamwagiza kutorudi tena kijijini, akimaanisha kutorudi kwenye mazingira yatakayomfanya aendelee kuwa kipofu na mfungwa wa fikra kama “wanyamugi” wengine na kutokupokea Habari Njema. Kwa hoja hiyo, hata Yesu mwenyewe hakuanza kazi kijijini Nazareti, badala yake akaenda Kafarnaumu ambako kumekucha na watu wake wamefunguka akili ya kupokea mambo mapya.

Wanakijiji wa Nazareti walimngoja Masiha atakayefuata mila na desturi zao yaani masiha anayeleta baraka iliyotangazwa na Mungu kwa Abrahamu kwa Waisraeli tu, wanaoshika vizuri utamaduni na mapokeo yao. Ili kuweza kuelewa zaidi maana ya kushika mila na desturi turejee kwenye jina wanalomwita Yesu baada ya kumshangaa wakasema: “huyu siye mwana wa Yusufu?” Katika utamaduni wa Wayahudi hata katika utamaduni wa Wabantu, mtoto anafanana na baba yake katika matendo, hasahasa katika thamani za kiutu anazorithi toka kwa Baba, kama wanavyosema: “mtoto amerithi tabia ya baba yake.” Waisraeli wanamshangaa Yesu kwa sababu walimwelewa baba yake Yusufu kuwa mtu wa haki, anayefuata Torah na mapokeo ya kijiji kama ilivyoandikwa kuwa “kila mwaka, yeye na familia nzima walienda Yerusalemu kuhiji.” Kwa hiyo wanamshangaa, kuwa inawezekanaje mwana huyu kutofanana na baba yake aliye mtu wa haki. Sifa hii ya haki ni sawa na neema, yenye maana pia ya uzuri, wema, utamu.

Sifa ya neema ilitokana na alichokisoma Yesu: “kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, yaani  kutangaza mwaka wa jubilei, mwaka wa neema, ambapo kulikuwa na lembuka ya bure kwa watu wote. Kwa hiyo Yusufu mwenye haki anawawakilisha Waisraeli wanaotakiwa kupata hiyo neema, na lembuka ya upendo wa Mungu kwa sababu wao ndiyo wenye haki. “Mtu mwenye haki atastawi kama mtende.” Ndiyo maana Waisraeli hapa wanashtuka na kushangaa maneno ya neema yaliyotakiwa kumwelekea mtu wa haki anayefuata mapokeo kama Yusufu: “wakayastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake,” wakabaki kujiuliza:“Huyu siye mwana wa Yusufu?”

Maneno yake ya neema, yalibidi yatoe ujumbe wa Masiha, mtawala, mshindi. Kumbe, wakazi wa Nazareti walistaajabia juu ya neno hili la neema, lililotoka mdomoni mwa Yesu wakitegemea kuwa sasa wabaya wote watalipwa kisasi. Wasikilizaji walitegemea Yesu angemalizia kusoma pale panaposema: “na siku ya kisasi cha Mungu wetu.” Kumbe Yesu akawapiga chenga, kwa makusudi kabisa “akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi.” Basi kutokana fikra zao finyu, Yesu akaona awatolee uvivu kwa kuwaelewesha juu ya neema ya bure ya Mungu na juu ya mtu mwenye haki, kwa mithali mbili zilizowatibua zaidi: “Hapana shaka mtaniambia mithali hii, “Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yao mwenyewe.” Hapa yaonekana kuwa watu wa Nazareti hawakuafiki kabisa kuwa mtoto wao anatoka kijijini kwao na kwenda mjini Kafarnaumu ulio mji wa kibiashara, mji wa kipagani, usioshika mila na utamaduni, na huko anaendesha lembuka ya bure kwa watu wasiostahili.

Mithali ya pili akawatolea mfano wa miujiza iliyofanyika kwa wapagani, akiwanukuu Manabii Eliya na Elisha, kuwa ndio anaowaiga kwani waliwaendea watu wapagani na wageni na kufanya lembuka ya bure, kwa sababu ujumbe wa neema na baraka ya Yesu ni kwa ajili ya watu wote. Kisha anahitimisha: “amin, nawaambia ya kwamba, hakuna Nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.”  Kwamba, Wanazareti walimtaka Yesu akiwa kama mtoto wa nyumbani na wa familia yenye kushika mapokeo, angeongea kile wanachotegemea wasikilizaji.

Ndugu zangu, kishawishi cha kutopokea ujumbe mpya wa neema upo pia mioyoni mwetu. Leo watu wanamtaka mhubiri aseme wanachokitaka kukisikia kadiri ya fikra zao. Yesu anatoa fundisho kwa wahubiri wote kwamba yabidi kuhubiri Habari njema, na siyo kufuata fikra zinazokubalika na mashabiki tu au kile wanachosubiri watu kusikia hata kama hakitokani na Mungu. Wakati mwingine ujumbe wa Kristu unaweza kuchokoza fikra za watu na kuwatibua nyongo kama ulivyokuwa ujumbe wa Yesu wa upendo usio na mipaka ulivyowachefua waumini ndani ya Sinagogi.

Hatima inasema kwamba: “Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukongo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.” Kitendo cha Yesu kufifia mbele za watu siyo suala la muujiza bali ni ujumbe wa matumaini unaowafariji wakristo wale waaminifu, kwamba wakitegemea ulinzi wa Kristu, wanaweza kupita bila shida na wasiwasi katikati madhulumu na kuendelea kwa uhakika na usalama kupeleka ujumbe wa mwalimu katika usafi na ukamilifu wake kwa watu wote.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.