2016-01-26 08:44:00

Papa Francisko ahimiza Wakristo kutembea njia ya Umoja


Jumanne jioni akiongoza Ibada ya Masifu ya Jioni  katika Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya Kuta  mjini Roma,  Papa Francisko, alihimiza Wakristo kutembea katika njia ya huruma na msamaha, kusahau makosa ya nyuma na badala yake wasonge mbele  kwa pamoja katika njia ya umoja. Aliomba kutoruhusu makosa ya nyuma kuendelea kuchafua uhusiano kati ya Wakristo.  Papa alieleza hilo wakati  akiongoza  sala za jioni,  kwa nia ya kuhitimisha Wiki la  Kuombea Umoja wa Wakristo, ambalo kila mwaka huanza tarehe 18 -25 Januari.

Katika hotuba yake,  Baba Mtakatifu alilenga zaidi katika  haja ya jumuiya za Kikristo zilizotengana, kujenga umoja na  kutembea pamoja katika njia ya Bwana kwa utambuzi kwamba, umoja ni zawadi toka mbinguni na katika uelewa kwamba, huduma zote zinazotolewa katika jina la Injili  ni kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa moja la Kweli kwa  utukufu wa Bwana mmoja, Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu alieleza na kupendekeza kwamba ”wakati wa  safari hii ya pamoja kuelekea ushirika kamili, kunaweza   anzishwa  mwendelezo wa  aina nyingi za ushirikiano, katika  neema kueneza Injili - na katika kutembea pamoja kwa  utambuzi kwamba, tayari tumeungana katika jina la Bwana."

Baba Mtakatifu aliendelea kutafakari umoja wa Wakristo akiangalisha pia katika uwepo wa Maadhimisho ya Jubilee ya Mwaka Mtakatifu, akisema yeye kama Askofu wa Roma, alipenda kuomba msahama kwa niaba ya Wakatoliki  kwa utendaji wa Wakatoliki, ulioumiza  Wakristo wa makanisa mengine, kinyume na  maadili  ya Injili.  Na wakati huo huo,  akawaomba Wakatoliki wote kusamehe  makosa yaliyofanywa  na Wakristo wa madehebu mengine  dhidi yao, iwe  nyakati hizi  au siku za nyuma . Alikumbusha katika Maadhimisho ya Jubilee hii maalum ya Mwaka Mtakatifu wa kuomba Huruma ya Mungu , ni lazima daima kukumbuka kwamba, hapawezi kuwa na mchakato wa kweli wa kujenga Umoja wa Wakristo bila kutegemea kikamilifu  huruma ya Baba.  Na kwamba ni tu huruma ya Mungu,  inayoweza kujenga uhusiano mpya kati ya Wakristo.

Baba Mtakatifu alieleza hayo  mbele ya umati mkubwa wa waamini wakiwemo wawakilishi kutoka makanisa mengine  na jumuiya , waliohudhuria Ibada hiyo kwa ajili ya kukamilisha Wiki ya Kuombea Umoja wa Wakristo. Kati yao, alikuwepo Mwakilishi kutoka Kansia la Kiotodosi  Askofu Mkuu wa Gennadionsi aliyewakilisha Upatriaki wa Kiekumeni , na Askofu Mkuu David Moxon wa  Kanisa la Kianglikan. Mwanzo wa  Ibada Papa aliwaalika wajiunge nae kutembea pamoja kupita Mlango Mtakatifu wa Kanisa la Mtakatifu Paulo nje ya kuta.  Papa Francisko amesisitiza kwamba , inawezekana kufanya maendeleo katika njia  wazi  za ushirika kamili, si tu wakati wa mikutano au wakati kunapokuwa na haja ya kukutana ana kwa ana ,  lakini juu ya yote, kupitia uongofu aminifu wenye kutuweka  karibu  zaidi na Bwana. 








All the contents on this site are copyrighted ©.