2016-01-25 11:45:00

Uchaguzi mkuu kurudiwa Visiwani Zanzibar tarehe 20 Machi 2016


Tume ya uchaguzi Visiwani Zanzibar inasema kwamba, wananchi Visiwani Zanzibar watafanya uchaguzi mkuu wa marudio hapo tarehe 20 Machi 2016, kufuatia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani uliofanyika kunako tarehe 25 Oktoba 2015. Maandalizi ya uchaguzi mkuu wa marudio yanaendelea vyema na kwamba, wananchi wanahamasishwa kushiriki kikamilifu, ili kukata mzizi wa fitina ambao umeiweka Zanzibar katika hali tete kisiasa. Matokeo ya uchaguzi mkuu yalifutwa kutokana na kasoro nyingi zilizojitokeza wakati wa uchaguzi, jambo ambalo lilipingwa na Chama cha Wananchi CUF.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha anasema, Serikali inaendelea kuimarisha ulinzi na usalama ili kuwahakikishia wananchi wote wa Zanzibar usalama wakati wote wa zoezi la uchaguzi mkuu wa marudio. Chama cha Wananchi CUF kimeonesha nia ya kutaka kususia uchaguzi mkuu, jambo ambalo linaweza kuleta mtafaruku mkubwa Visiwani Zanzibar. Wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuhamasishwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa marudio, ili kudumisha demokrasia na haki ya wananchi Kikatiba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.