2016-01-25 06:55:00

Mageuzi mbele kwa mbele: kielelezo cha ujasiri wa kinabii!


Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari, inafunga pia Juma la kuombea Umoja wa Wakristo ambalo kwa mwaka huu 2016 limeongozwa na kauli mbiu “Mpate kuzitangaza fadhili za Mungu”. Itakumbukwa kwamba, sala na tafakari za juma la kuombea Umoja wa Wakristo ziliandaliwa na Jumuiya ya Wakristo kutoka Lithuania. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kiekumene uliopewa msukumo wa pekee na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Askofu mkuu Brian Farrel, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, changamoto kubwa iliyoko mbele ya Makanisa kwa wakati huu ni umoja wa Wakristo, ili kushuhudia Injili ya Kristo inayojikita katika uhalisia wa maisha. Haya ni majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika ukweli, upendo, sala na damu ya mashuhuda wa Injili kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Umefika wakati kwa Makanisa kuonesha ujasiri ili kuondokana na woga wa kutaka kushikamana na utambulisho wake kwa gharama ya umoja wa Wakristo.

Mwelekeo wa sasa wa majadiliano ya kiekumene, unatia moyo, kwani waamini wa Makanisa mbali mbali wanaweza kukutana na kusali pamoja, bila kuwa na wasi wasi wa waamini wenye misimamo mikali. Hapa jambo la msingi ni kutaka kukazia ufuasi, ari na mwamko wa kimissionari sanjari na ushuhuda wa huduma inayotolewa na Wakristo kwa familia ya Mungu. Hapa majadiliano ya kiekumene yanapata mwelekeo wa kiroho na kiutu, tayari kushuhudia umoja wa Kanisa kadiri ya mapenzi ya Kristo mwenyewe.

Ushuhuda wa kinabii ni dhana inayomwilishwa na watakatifu na familia ya Mungu inayojikita katika utakatifu wa maisha ili kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu kati ya watu wake, mahali ambapo Wakristo wote wanajisikia kuwa wako nyumbani, wanakubalika, wanapokelewa na kuthaminiwa. Katika mchakato wa mabadiliko na mageuzi ndani ya Kanisa, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanalitaka Kanisa kuendelea kua aminifu katika maisha na utume wake kwa kuthamini na kuendeleza amana ya imani.

Mageuzi ya Kanisa yanajikita kwa namna ya pekee katika: Liturujia, Sheria za Kanisa, Sera na Mikakati ya shughuli za kichungaji. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, kumekuwepo na mafanikio makubwa, lakini hata hivyo bado kuna mambo mengi yanayopaswa kufanyiwa kazi na Makanisa, ili kufikia umoja kamili kadiri ya mpango wa Yesu. Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuimarisha majadiliano ya kiekumene kwa kukazia dhana ya Kanisa kadiri ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amekutana na kuzungumza na waamini wa Makanisa mbali mbali ya Kikristo, amewatembelea na kusali pamoja nao, mambo msingi yanayodumisha majadiliano ya kiekumene katika uhalisia wa maisha. Hivi karibuni, Makatibu wakuu wa Jumuiya za Kikristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia walikutana mjini Londona, Uingereza, pamoja na mambo mengine, wamemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kwamba, kwa mwelekeo kama huu, kuna uwezekano kabisa wa kufikia umoja kamili ndani ya Kanisa la Kristo.

Askofu mkuu Brian Farrel anasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutekeleza dhamana ya utume wa kinabii ili kulisha na kurutubisha matumaini ya mwelekeo mpya katika maisha na utume wa Kanisa. Ubatizo, Injili na Imani kwa Kristo Yesu ni mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo waliogawanyika kutokana na matukio mbali mbali ya kihistoria ndani na nje ya Kanisa. Changamoto kwa Wakristo wote ni kushuhudia Injili ya Kristo katika mchakato wa Uinjilishaji mpya pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu Francisko anaonesha ari na mwamko mpya wa kutaka kuleta mabadiliko makubwa katika umoja na mshikamano wa Kanisa kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Katika mageuzi yanayofanywa na Baba Mtakatifu kwa wakati huu ni dhana ya uongozi wa Kanisa unaopaswa kujikita katika dhana ya “Sinodi” katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia hii anataka kuimarisha urika wa Maaskofu katika kukabiliana na majukumu mbali mbali ndani na nje ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuonesha umoja, mshikamano na urika wa maaskofu wote ili kukuza mwelekeo kadiri ya mafundisho tanzu ya Kanisa pamoja na kuendelea kuhamasisha ari na mwamko wa kimissionari. Kwa Makanisa mahalia, Baba Mtakatifu anaendelea kutoa mwaliko kwa Maaskofu kutambua na kuthamini wajibu wao msingi kuwa wao ndio wachungaji wakuu wa waamini waliokabidhiwa kwao na Kanisa na kutokana na mamlaka haya, Askofu pia ni Hakimu wa watu wake anayepaswa kuangalia hata masuala ya ndoa na familia, dhamana ambayo sehemu kubwa ya Kanisa inatekelezwa na viongozi waliopewa dhamana na Maaskofu mahalia.

Mahakama ya Kanisa kikanda ni utekelezaji wa dhana ya Sinodi ndani ya Kanisa. Maaskofu wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wao. Kumbe, kwa kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko uongozi ndani ya Kanisa ni dhana shirikishi. Hizi ni tunu ambazo zimekuwepo katika maisha na utume wa Kanisa, sasa umefika wakati wa kuhakikisha kwamba, zinamwilishwa na kufanyiwa kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Askofu ni mdhamini na mrithishaji wa Mapokeo ya Kanisa anayepaswa kuwa na umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro kielelezo cha umoja, imani na upendo ndani ya Kanisa.

Makanisa mbali mbali ya Kikristo yanaangalia mabadiliko yanayoletwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa kwa moyo wa shukrani na matumaini makubwa katika mchakato wa kufikia umoja kamili wa Kanisa. Dhana ya Sinodi, mageuzi na mabadiliko ndani ya Kanisa ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kwa kuzingatia utume wa kinabii, ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kusali na kumwilisha mapenzi ya Kristo Yesu pasi na wasi wasi wala mashaka, ili wote waweze kuwa wamoja, na ulimwengu upate kuamini kwamba, Kristo ametumwa na Baba yake wa mbinguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.