2016-01-25 09:39:00

Elimu makini ni chachu ya majadiliano ya kidini!


Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Dhamana ya Afrika, Africae munus anasema kwamba majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwani hili ni suala changamani. Hizi zinapaswa kuwa ni juhudi za mshikamano wa upendo unaojikita katika uhalisia wa maisha ya watu ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho.

Jamii haina budi kuondokana na aina zote za ubaguzi kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wa dini mbali mbali hawana budi kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu msingi wa haki zote za binadamu. Uhuru wa kidini ni njia inayowaelekeza wanadamu katika haki, amani na maridhiano.

Mababa wa Sinodi ya Afrika wanatambua na kuthamini mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu, inayowawezesha watu kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni na kimaadili. Kanisa Barani Afrika kwa miaka mingi limeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuwasaidia watu kutambua ukweli ili kuweza kuumwilisha katika vipaumbele vyao vya maisha.

Askofu Joseph Alessandro wa Jimbo Katoliki Garissa, nchini Kenya katika mahojiano maalum na Kituo cha Radio Waumini, kinachomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Kenya anasema, moja ya mikakati yake ya shughuli za kichungaji Jimboni Garissa ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam kwa njia ya elimu makini inayogusa mtu mzima: kiroho na kimwili. Lengo ni kuvunjilia mbali misimamo mikali ya kidini, inayojengeka kwa misingi ya ubaguzi; kukata mzizi wa fitina unaojificha katika ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Kenya. Elimu ndio ufunguo wa maendeleo na ustawi wa wengi.

Askofu Alessandro aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Garissa, eneo ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa ni uwanja wa fujo, kwa masikitiko makubwa anasema, Garissa ni eneo ambalo limebaki nyumba kimaendeleo kwa kukosa miundo mbinu makini ya shule, afya na usalama kutokana na hofu za mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na kikundi cha Al Shabaab kutoka Somalia. Ukosefu wa ulinzi na usalam umewafanya wazazi na walezi wengi kuwaondoa watoto wao katika shule zilizoko Garissa na kuwatafutia sehemu nyingine.

Askofu Alessandro anasema hofu, wasi wasi na mashaka vinaweza kuondoka miongoni mwa wananchi kwa kujikita katika elimu bora na makini, inayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ndiyo maana anaiomba familia ya Mungu nchini Kenya kumuunga mkono kwa hali na mali, ili kuwekeza katika sekta ya elimu, ili kuwawezesha wanafunzi kurejea tena darasani; kuwawezesha watu kupata huduma ya afya pamoja na kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Mambo yote haya ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Jimbo Katoliki la Garissa linataka kuwekeza katika elimu kama chombo cha majadiliano ya kidini. Kwa sasa Jimbo linaendesha na kumiliki shule tano za msingi pamoja na shule za awali nane; kituo cha afya pamoja na kituo cha walemavu.

Habari na Rose Achiego na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.