2016-01-23 14:49:00

Waonjesheni watu muujiza wa huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Maaskofu Katoliki Ufilippini kutafuta mbinu na njia mpya ya kutangaza na kuhudhudia muujiza wa huruma ya Mungu kati ya watu wao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Askofu mkuu Giuseppe Pinto, Balozi wa Vatican nchini Ufilippini wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya kufungua Mkutano wa mia moja na kumi na mbili wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, Ijumaa, tarehe 22 Januari 2016.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anaendelea kukazia dhamana na utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu ambayo ni endelevu kwa waja wake. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi kukaza ya macho, akili na mioyo kwa huruma ya Mungu, ili iweze kuwagusa watu wengi katika maisha na utume wao.

Baraza la Maaskofu Katoliki linafanya mkutano huu, wakati linajiandaa pia kufungua maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, linaloanza kutimua vumbi,  Jumapili, tarehe 24 hadi 31 Januari 2016, Jimbo kuu la Cebu, linaongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu”. Huu ni mchakato wa unaopania kukuza na kudumisha Uinjilishaji mpya unaojikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni sanjari na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Wakristo wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, mapendo na huruma ya Mungu kwa jirani zao, hususan wanaposhiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kanisa lisimame kidete kuwahudumia, kuwatetea na kuwafariji maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii Barani Asia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.