2016-01-23 11:17:00

SECAM: Sera na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji Afrika


Kutokana na vita, kinzani za kijamii, kisiasa na kidini; umaskini, njaa na maradhi; nyanyaso na dhuluma mbali mbali, wananchi wengi Barani Afrika wamejikuta wakilazimika kuyakimbia makazi yao, ili kutafuta hifadhi na usalama ndani na nje ya Bara la Afrika. Kwa bahati mbaya, wakimbizi na wahamiaji hawa wamekuwa wakikabiliana na kifo uso kwa uso wanapokuwa njiani kuelekea kwenye nchi zilizojaa maziwa na asali! Ni makundi yanayokumbana na ukatili wa ajabu pamoja na sheria kandamizi; hali ambayo inapelekea wakimbizi na wahamiaji wengi kuishi katika mashaka na hali ya kudhaniwa vibaya.

Mwelekeo kama huu aliwahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kichungaji Dhamana ya Afrika, Africae munus, huamsha matendo ya kutovumiliana, chuki na ubaguzi kwa wageni na wahamiaji; dhuluma na nyanyaso. Kanisa linapenda kutoa changamoto ya pekee kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji kwa kuonesha mshikamano wa upendo; kwa kuwapatia mahali salama panapoweza kuwakirimia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kanisa litaendelea kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia wakimbizi kwa kuwaonesha ile sura ya Huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao, hususan mwaka huu Mama Kanisa anpoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kwa kutambua uzito na changamoto za wakimbizi na wahamiaji Barani Afrika, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linaendesha mkutano kuhusu wakimbizi na wahamiaji Barani Afrika; mkutano ambao unafanyika Brazzavile, Jamhuri ya Watu wa Congo. Lengo ni kutafuta na kutunga sera na mikakati itakayosaidia kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika. Huu ni mkutano wa kwanza kimataifa unaojadili pia taalimungu ya wahamiaji Barani Afrika. Wawakilishi kutoka katika Nchi za SECAM wanahudhuria.

Askofu Miguel Olaverri, Mwenyekiti wa Tume ya Wakimbizi na Wahamiaji Baraza la Maaskofu Katoliki Congo katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu amewakumbusha wajumbe kwamba, hata leo hii kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaohatarisha amani, usalama na mafungamano ya kijamii kutokana na uchu wa mali na madaraka; matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Kanisa Barani Afrika halina budi kukita mizizi yake katika huruma ya Mungu, upendo, mshikamano na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Hii ndiyo changamoto kubwa ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameliachia Kanisa Barani Afrika alipotembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, akaonesha na kushuhudia nguvu ya imani inayovuka mipaka ya woga na wasi wasi.

Kwa upande wake, Askofu Louis Portella Mbuyu, Makamu wa Rais wa SECAM, kwa namna ya pekee, anaialika Familia ya Mungu Barani Afrika kujikita katika dhamiri nyofu, tayari kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; binadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa lijiwekee sera na mikakati kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, walau mambo yanayopelekea watu kukimbia nchi zao yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu, ili haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu yaweze kutawala katika akili na mioyo ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.