2016-01-23 15:28:00

Mafanikio, matatizo na changamoto za majadiliano ya kidini


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini anapenda kufanya tafakari ya kina kuhusu mambo msingi yaliyojitokeza kwa mwaka 2015 na mwelekeo wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika kipindi cha mwaka 2016. Anasema, mwaka 2015 umesheheni matukio ya kusikitisha kutokana na vita, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa sehemu mbali mbali za dunia.

Matukio kama haya yanaweza kuhatarisha na hatimaye, kukwamisha mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali. Lakini, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, hapa ndipo wanapotakiwa kusimama kidete kuendeleza majadiliano ya kidini, ili haki, amani na  maridhiano yaweze kutawala katika akili na miyo ya watu kwa kuheshimiana na kuthaminiana na kwamba, tofauti zao za kidini si sababu msingi ya kuleta vita na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Majadiliano ya kidini ni mchakato usiokuwa na mbadala miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali.

Licha ya matukio haya ya kusikitisha na kukatisha tamaa, lakini pia kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani. Katekisimu ya Kanisa Katoliki ambayo ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala imetafsiriwa katika lugha ya “Farsi” na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali na kuzinduliwa kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma.

Kwa mara ya nne, kuna maandalizi ya mkutano kati ya Wakristo na Waislam, utakaofanyika huko Teheran, mwezi Desemba 2016. Mwezi Februari kutafanyika mkutano kati ya Wakristo na Waislam; mkutano ambao ulitarajiwa kufanyika mjini Roma, Mwezi Novemba, 2015, lakini kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika, mkutano huu sasa unatarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2016.

Mwezi Septemba 2015, Baraza la Kipapa limeshiriki katika mkutano uliowaunganisha Wakristo na Waislam huko Argentina, ili kuhamasisha utamaduni wa kuheshimiana na mshikamano kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani. Mkutano huu ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Jukwaa la Viongozi wa Utamadauni wa Kiislam kutoka Amerika ya Kusini na Caribbean.

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini limeendelea kutoa ujumbe wa matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Id Al Firtri, inayohitimisha Mfungo wa Mwezi  Mtukufu wa Ramadhan, kwa kuwataka waamini wa dini hizi mbili, kujifunga kibwebwe kusimamia misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kukataa kishawishi cha kutumia dini kama chombo cha vita, mauaji na mipasuko ya kidini ndani ya jamii.

Ujumbe huu, uliungwa mkono na waamini wengi, hususan viongozi wa kisiasa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaotaka kuona haki, amani, utulivu, upendo, mshikamano na maridhiano yanatawala kati ya watu wa mataifa. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini limeendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali za dini ya Kiislam katika mchakato wa kudumisha majadiliano ya kidini, ili kudumisha maridhiano na uelewano kati ya watu.

Kardinali Tauran anaendelea kufafanua kwamba, katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko juu la majadiliano ya Kidini, Nostra aetate, umekuwa ni ushuhuda makini kwamba, ikiwa kama waamini na watu wote wenye mapenzi mema wataonesha utashi na kukumbatia ukweli na uwazi; amani na maridhiano, vikwazo vingi vinavyozorotesha mahusiano ya waamini wa dini hizi mbili vinaweza kupatiwa ufumbuzi.

Umoja na ushirikiano na Wayahudi pia umepewa mkazo wa pekee katika kipindi cha mwaka 2015 na kwamba, Kanisa linaendelea kushiriki kikamilifu katika mikutano na mikakati inayopangwa na Kituo cha Kimataifa cha Majadiliano ya Kidini, (Kaiciid) chenye makao yake makuu mjini Vienna, ili kudumisha amani duniani, maelewano pamoja na majiundo makini ya watu wa dini mbali mbali kukutana na kujenga madaraja ya ushirikiano. Viongozi wa kisiasa nao wanaendelea kuunga mkono juhudi za ujenzi wa misingi ya amani na utulivu.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika ilikazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Majadiliano haya yajikite katika fadhila ya ukweli, upendo na huduma. Mwezi Mei, 2016 huko Washington, DC, kutafanyika mkutano na waamini wa dini ya Kihindu na Kijainisti; hawa ni wale wanaoishi nchini Marekani.

Mwezi Februari 2015 huko Bodh Gaya, India kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki India, kulifanyika mkutano wa amani kwa kuwashirikisha viongozi wa dini ya Kibudha, ili kudumisha mshikamano pamoja na kusimama kidete kupinga utumwa mamboleo, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mambo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; pamoja na kushikamana ili kudumisha udugu, upendo na amani duniani.

Kardinali Jean Louis Tauran anasema, majadiliano ya kidini ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto inayowahusisha hata viongozi wa kisiasa ili kuondokana na woga usiokuwa na mashiko ili kutambua mchango wa dini katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Pili kuna changamoto ya kiakili inayowataka waamini wa dini mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatumia hazina kubwa ya kitaalimungu, ili kujenga mazingira ya kukutana na watu wa nyakati hizi.

Tatu ni changamoto ya maisha ya kiroho, inayowataka waamini wa dini mbali mbali kutambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano, wanaotakiwa kujenga na kudumisha umoja na udugu; upendo na ukarimu, toba na msamaha wa kweli! Haki msingi za binadamu, utu na heshima yake ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee na waamini wa dini mbali mbali duniani. Waamini wawe waaminifu kwa mafundisho tanzu ya dini zao kwa kuepuka misimamo mikali ya kiimani ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao.

Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ni jambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini ni mchakato wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi; katika haki na amani; upendo na udugu. Waamini wanapaswa kujenga tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana na wala hakuna sababu ya kuogopana, ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa wale waliokata tamaa anasema Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika tafakari yake inayochambua mafanikio, matatizo, changamoto na fursa za maboresho ya majadiliano ya kidini kwa mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.