2016-01-23 09:39:00

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete dhidi ya mauaji ya kimbari!


Monsinyo Janusz Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa Vienna, Austria anasema, Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 27 Januari 2016 itaadhimisha kumbu kumbu ya wahanga wa mauaji ya Shoah yaliyoplekea maelfu ya watu kuuwawa kikatiliki, lakini pia Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kukumbuka mauaji ya kimbari na ukatili uliofanywa dhidi ya makundi mbali mbali ya watu, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya kila binadamu.

Monsinyo  Urbanczyk ameyasema haya hivi karibuni wakati alipokuwa akichangia katika mkutano wa Baraza kuu la OSCE katika kikao chake cha laki moja na themanini na sita elfu. Watu wote wanapaswa kutambua kwamba, kwa pamoja wanaunda familia kubwa ya binadamu; kwa kutambuana kama ndugu na jirani na wala si tena wageni wala watu wa kuja! Hapa, Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kupinga kwa nguvu zote sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo dhidi ya maisha, utu na heshima ya binadamu.

Monsinyo Urbanczyk anakaza kusema, vita, mashambulizi na mauaji ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia; mambo ambayo wakati mwingine yanatendwa ka kisingizio cha jina la Mwenyezi Mungu, yanapaswa kudhibitiwa na kuwafikisha wahusika kwenye mkondo wa sheria. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya uhai, utu na heshima ya binadamu, kamwe hawezi kuwa ni chanzo cha utamaduni wa kifo, hii ni kufuru ya kidini inayotumiwa na baadhi ya waamini kuhalalisha mauaji ya kinyama kwa watu wasiokuwa na hatia.

Binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wanatofautina kwa mambo mengi lakini wote wanakamilishana katika utofauti wao ambao ni utajiri mkubwa machoni pa Mwenyezi Mungu. Kanisa Katoliki linaendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani. Vatican inapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano pamoja na uhuru wa kuabudu msingi wa haki nyingine zote za binadamu. Historia ya mambo yaliyopita isaidie Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini kwa sasa na kwa siku za usoni, ili kujenga na kudumisha udugu, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.