2016-01-22 10:46:00

Ndoto ya Mungu katika Ndoa Takatifu: Udumifu, upendo, mshikamano na uumbaji!


Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki “Rota Romana” ni mahakama ya familia; Mahakama ya ukweli na vifungo vya maisha matakatifu na ni chombo muhimu sana kinachomwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza wajibu wake barabara ndani ya Kanisa, tayari kutangaza Mpango wa Mungu Muumbaji na Mkombozi kuhusu uzuri na utakatifu wa maisha ya familia. Kanisa linapenda kuendelea kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu, hususan kwa familia ambazo zimeguswa na kutikiswa na dhambi pamoja na kinzani za maisha, ili kwa pamoja, Watu wa Mungu waweze kutangaza ukweli wa ndoa kadiri ya Mpango wa Mungu. Hii ni dhamana ambayo amekabidhiwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Maaskofu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 22 Januari 2016 alipokutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Mahakama kuu ya Rufaa, kama sehemu ya uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama mjini Vatican. Familia ni mada ambayo imechambuliwa hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya familia, kwa kujikita katika urika wa Maaskofu kiasi cha kukazia kwa mara nyingine tena dhana ya familia kadiri ya Mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Mahakama kuu ya Rufaa inapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia mwelekeo wa maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji, katika kutoa hukumu na kufunda dhamiri za watu ili waweze kuufahamu ukweli. Kanisa daima linataka kutangaza ukweli kuhusu Ndoa, kwa ajili ya ustawi na mafao ya waamini bila kuwasahau wale wanaoteseka kutokana na kinzani za kifamilia, ili wao pia waweze kuonja huruma ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndoa isiyotenguliwa inayojikita katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati; ndoa inayopania kuendeleza kazi ya uumbaji, hii ndiyo ndoto ya Mwenyezi Mungu kwa Kanisa na wokovu wa binadamu. Kanisa limeendelea kuwa na jicho la huruma kwa familia ambazo zinaogelea katika shida na mahangaiko mbali mbali. Kwa njia ya Ndoa Takatifu, Mwenyezi Mungu amependa kuunganisha mambo makuu mawili: utume wa kurithisha maisha; upendo na muungano wa dhati kati ya bwana na bibi wanaokamilishana kiroho na kimwili.

Kwa njia ya Ndoa Takatifu, Mungu anawawezesha wanandoa kushiriki katika upendo wake na kuwahamasisha ili waweze kusaidiana na kujitosa bila ya kujibakiza kati yao, ili kufikia utimilifu wa maisha. Upendo huu kwa binadamu ni chachu inayomshirikisha mwanadamu maisha na furaha ya uzima wa milele. Familia na Kanisa ni taasisi mbili muhimu zinazopenda kumsindikiza mwanadamu ili kufikia mwisho wa maisha yake. Taasisi hizi zinatekeleza dhamana na utume huu kwa njia ya Mafundisho tanzu pamoja na kuendeleza Jumuiya ya upendo na maisha.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani na Watu wa Mungu; ni nguzo msingi wa Kanisa na kwamba,  tangu sasa wao si wageni wala wapitaji, bali ni wenyeji, watakatifu na watu wa nyumbani kwake Mungu. Kanisa linatambua kwamba, ni Mama na Mwalimu; kati ya watoto wake kuna wale wenye imani thabiti wanaojikita katika upendo unaoimarishwa na kudumishwa kwa njia ya katekesi makini na kurutubishwa kwa sala na Sakramenti za Kanisa; lakini pia kuna watoto wake ambao wako hoi bin taabani, imani yao inachechemea; hawakupata malezi makini au pengine wamesahaulika.

Baba Mtakatifu anakaza kusema ubora wa imani si sifa muhimu sana kwa ajili ya maisha ya ndoa kwani ikiwa kama mwamini hakupata majiundo makini, imani hii inaweza kuonekana kana kwamba inakosekana. Kuna baadhi ya wanandoa ambao wanapochukua maamuzi magumu ya kufunga ndoa hawana uelewa makini wa Mpango wa Mungu katika maisha yao, lakini baadaye katika maisha ya kifamilia wanamgundua Mungu kuwa ni Muumbaji na Mkombozi.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ukosefu wa majiundo makini ya imani na kutofahamika kwa mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia, kama vile: umoja, udumifu, utakatifu na uzuri wa Sakramenti ya Ndoa ni mambo ambayo yanaharibu maridhiano na utashi wa maisha ya ndoa. Makosa haya yanayoleta usumbufu katika Sakramenti ya Ndoa yanapaswa kupembuliwa kikamilifu. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwahamasha Wakristo kufunga ndoa kwa kukazia kwa namna ya pekee mambo yafuatayo: Uzazi; mafao ya wanandoa, umoja, udumifu na Sakramenti.

Hakuna ndoa ya mpito, bali kila mwamini kwa njia ya neema ya Kristo Yesu anaweza kuishi kikamilifu Sakramenti ya Ndoa. Hapa kuna haja ya kuweka sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazozishirikisha taasisi mbali mbali za Kanisa, ili kuwa na maandalizi makini kwa wanandoa watarajiwa kama walivyokazia Mababa wa Sinodi ya familia. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa wafanyakazi wa Mahakama kuu ya Rufaa mjini Vatican kwa kuwakumbusha kwamba, hizi ni nyakati ambazo Familia na Kanisa linapaswa kuwajibika zaidi ili kuwasaidia wanandoa katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu anawatakia wote heri na baraka kwa Mwaka mpya pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, ili Kanisa liweze kukuza ari na moyo wa familia na kwa upande wake, familia zijisikie kuwa kweli ni sehemu hai ya Watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.