2016-01-22 07:26:00

Huo si mchapo uliozagaa kama magazeti ya Udaku!


Kuna sehemu nyingi zina masoko ya wazi, ambapo wafanya biashara wadogo wadogo hujenga vibanda na kutandaza bidhaa mbalimbali zikiwa ni pamoja na viwalo, vyakula, vinywaji, mifugo nk. Masoko hayo yanaitwa Lembuka au Mnada. Kwa kawaida katika Lembuka bidhaa huwa bei nafuu kidogo kulinganisha maduka ya kawaida. Leo tutaiona Lembuka moja iliyosheheni bidhaa nzuri na ya thamani kubwa, lakini ni bure hakuna kununua wala kuuza. Mtayarishaji wa Lembuka hiyo anawaalika wote kwenda kula, kunywa, na kununua bidhaa bila pesa kama asemavyo Nabii Isaya: “Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; naam, njoni, nunueni divai na maziwa, bila fedha na bila thamani.” (Isaya 55:1).

Injili inayotuongoza kwenye lembuka hiyo imegawanyika sehemu mbili: Sehemu ya kwanza ni matangulizi ya jumla yanayokuandaa kupokea mwaliko wa kwenda lembuka na sehemu ya pili ni mwaliko wenyewe wa kuingia Lembuka. Utangulizi umeandikwa kwa mtindo wa uandishi wa wakati huo. “Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu, kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo, nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo, mtukufu, upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.”

Waandishi walitumia safu ya utangulizi kuandika wazo au lengo kuu la uandishi. Aidha walimtaja aliyegharimia uandishi mzima. Hapa Mwinjili anamtaja Theofilo aliyekuwa Mkristo hodari wa jumuia ya Filipo. Mwandishi anakiri kuwa kulikuwa na watu wengi kwa kutumia akili zao, waliandika mambo mengi aliyosema na kutendwa na Yesu, na taarifa hizo zilizagaa kama magazeti ya udaku. Naye mwandishi wa Injili hii anaona aingize mkono wake kuandika habari hizo lakini siyo kama hadithi, mchapo au taarifa za kiakili, bali kwa mpangilio mzuri wa kinyaraka. Ameshakusanya taarifa mbalimbali kutoka kwa watu waliokuwa watumishi wa Neno hilo toka mwanzo.

Watu hao waliliishi na kulishuhudia Neno hilo katika maisha yao.  Mwinjili amevutwa na Neno hilo na anataka kumdhihirishia Theofilo kimaandishi ukweli na uzito wa mambo hayo na siyo kutegemea taarifa za udaku zilizoandikwa bila kuwa na mang’amuzi ya Neno hilo katika maisha. Kwa hiyo lengo lake siyo kuwaandikia wasiolijua Neno, la hasha bali kuwaandikia waamini wale walioliishi hilo Neno, ili kuwathibitishia kuwa imani yao imejengwa juu ya mwamba thabiti, na kwamba imani imejengwa katika kumuishi na kumshuhudia Yesu Kristo.

Baada ya Utandalizi huo, sasa tunaingizwa sehemu ya pili ambayo ni ujumbe wa mwaliko wa kuingia sehemu ya Lembuka. Yesu alitembelea kijijini alikolelewa ambako alitoa ujumbe huo maalumu: “Akaenda Nazareti hapo alipolelewa; na siku ya sababu akaingia katika sinagogi kama iivyokuwa desturi yake.” Suala la Yesu kurudi kijijini linasimuliwa na Injili pacha zote tatu yaani Mathayo, Marko na Luka.

Wainjili wawili wanamwonesha Yesu akiwa na wanafunzi wake anarudi nyumbani baada ya kuhubiri kwa muda mrefu huko Kafarnaumu. Lakini Luka peke yake kwa hoja ya kiteolojia anamwonesha Yesu anarudi kijijini mwanzoni tu mwa maisha yake ya hadharani. Kadhalika, ujumbe anaotoa kijijini kwake akiwa kwenye Sinagogi ni mwaliko mzito unaomhusu yeye na utume wake kama Masiha. Yesu alipokuwa kijijini kwake ikaangukia siku ya Sabato ambapo walikwenda kusali kwenye Sinagogi. Katika ibada hiyo kulikuwa na desturi ya kusoma Neno la Mungu toka katika Biblia. Kwa kawaida Neno lilichukuliwa toka moja ya kitabu cha Torati ya Musa au kitabu cha Manabii hasahasa Isaya. Kwa vile Nazareti kilikuwa kijiji kidogo, hapo kulikuwa na kitabu kimoja tu cha Nabii Isaya. Kwa bahati nzuri akakabidhiwa yeye kusoma kama ilivyoandikwa: Wakamkabidhi Maandiko Matakatifu.

Alipokabidhiwa, naye akafungua. Huko kufungua kunamaanisha kuwa, asingekuwa Yesu kufungua, hapo Andiko hilo litaendelea kubaki limefungwa. Aidha Neno hilo haliwezi kueleweka wala kukamilika bila kufunguliwa na Yesu. Yesu anasimama na anachagua kusoma aya mbili tu kwa sababu zinaeleza mada inayomhusu. “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” (Isaya 61:1-2b) Unabii huu wa mtu aliyetumwa na Mungu umejaa Roho Mtakatifu, kwa ajili ya kutangaza habari njema, ulitolewa na mtu asiyejulikana jina hapo miaka mia nne kabla ya Yesu.

Wakati huo watu walikuwa wanakatishwa tamaa, wanateswa, wananyamazishwa, wanakandamizwa, kunyanyaswa na hawakuweza kujitetea. Katika mazingira hayo alitegemewa kuja huyo Mpakwa wa Bwana na kuleta Habari Njema ya ukombozi kwa watu hao.  Yesu baada ya kufungua na kusoma ujumbe unaomhusu anafunga kitabu na kumrudishia mtumishi. Kisha akaketi kuonesha kuwa yeye sasa ndiye “Mwenyekiti wa mkutano” “Kigogo” na wengine wote wakabaki kumsikiliza. Ndipo akaona atumie fursa hiyo kutoa ujumbe wake, akasema: “Leo yametimilika maneno haya.” Tamko hili Leo linajirudia kuonesha kuwa ni kutoka pale Yesu alipoingiza habari njema kuwa ni mwanzo mpya. Leo kila mmoja katika mazingira mbalimbali Yesu anawaalika wote, walala hoi, wafungwa, vipofu, wanaokandamizwa katika jamii, waende kujimwaga kwenye lembuka.

Sifa na kazi za Yesu aliyetiwa mafuta na ambaye Roho wa Bwana yu juu yake ni: Mosi, “kuwahubiri maskini habari njema.” Habari njema kwa watu maskini ni ule upendo wa Mungu usio na mipaka. Kama vile kwa wale wachungaji waliotangaziwa Habari njema iliyowawezesha kuziishi ndoto zao za maisha. Pili, “kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao:” Yesu amefika kutengua, kulegeza, kufungua vifungo vinavyomzuia mtu asiweze kutembea. Kutufungua na vifungo vinavyotunyima uhuru wa mahusiano kati yetu na Mungu, yaani kutufungua na vifungo vinavyotuzuia kumpenda Mungu. Aidha amekuja kutufungua na vifungo vya ubinafsi vinavyotunyima uhuru wa mahusiano yetu na wenzetu. Zaidi tena tunakuwa huru kutokana na machungu, masikitiko, wivu na chuki tulizonazo dhidi ya wengine waliotutendea mabaya. Anatuweka huru na mambo yale yanayotufanya tuwe watumwa na mambo ya kale tusiweze kupokea Habari Njema. Hutufungua na vimungu vinavyotufanya tuwe wanafiki na tusiwe tunavyotakiwa tuwe.

Tatu, “vipofu kupata kuona tena:” Vipofu wako gizani na hawaoni mwanga. Yesu amekuja kutufungua macho ili tuweze kuona vizuri na kupambanua mambo. Nne,“kuwaacha huru waliosetwa:” Uhuru unaosemwa hapa siyo wa Isaya sura 61 bali ni kutoka Isaya 68, pale nabii anapozunguza juu ya mfungo anaotaka Mungu: “Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana. Je, kufunga namna hii ni saumu nilioichagua mimi? Je, ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake?” (Isaya 58:4-5) Kufunga anakotaka Mungu ndiko huku: “Je, saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa. Je, siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwona mtu aliye uchi, umvike ngo wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?” (Isaya 58:6-7) Hii ndiyo lembuka ya Yesu.

Jambo la tano na la mwisho ndilo pendo la bure, nalo ni “kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Mwaka wa Bwana ulikuwa ni mwaka wa jubilei. Mwaka wa jubilei ulikuwa kila baada ya miaka saba. Katika mwaka wa jubilei mambo yalikuwa chekwachekwa. Kila mmoja alipata fursa ya kuwa na haki yake na kumiliki mali yake. Tabia au Roho pekee ya Mungu inayoonekana katika Yesu ni ile ya kuona na kupokea upendo wa bure wa Mungu. Mwaka wa jubilei au mwaka wa neema, ni mwaka wa upendo wa bure. Tukiingia katika upendo wa bure wa Mungu tutaushirikisha pia bure kwa wengine. “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu.”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.