2016-01-22 11:28:00

Askofu ni nguzo ya Kanisa, lakini asiye sali ni janga kwa watu wa Mungu!


Askofu anayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao. Ili kutekeleza vyema dhamana hii, Askofu hana budi kuwa kweli ni mtu wa sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu, tayari kusimama kidete kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Askofu ambaye ni mvivu katika maisha ya sala, huyo atasababisha majanga kwa watu wa Mungu. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 22 Januari 2016 katika Ibada ya Misa Takatifu alioiadhimisha kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican.

Tafakari ya Baba Mtakatifu imechota utajiri wake katika Injili ya Siku, Yesu anapowachagua Mitume wake kumi na wawili ili wapate kuwa pamoja naye na kwamba, awatume kuhubiri pamoja na kuwa naamri ya kutoa pepo. Mitume wa Yesu walikuwa ni Maaskofu wa kwanza walioteuliwa na Yes una baada ya kifo cha Yuda Iskarioti, Mathayo akateuliwa kuwa pia Mtume wa Yesu na kuwa Askofu wa kwanza kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa. Maaskofu ni nguzo ya Kanisa wanaopaswa kuwa ni mashuhuda wa Ufufuko wa Kristo pamoja na matumaini kwa Kristo anayekarimu na kusamehe. Ushuhuda wa Maaskofu hauna budi kujikita katika uhalisia wa maisha.

Maaskofu hawana budi kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mahusiano ya karibu na Yesu kwa njia ya Sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Wajibu wa pili wa Askofu ni kuwa shuhuda wa Kristo Mfufuka; mambo msingi yanayolitegemeza Kanisa la Kristo. Nguzo hizi zitayumba, ikiwa kama zitakosa nguvu ya sala na tafakari ya Neno la Mungu na matokeo yake, zitakuwa ni majanga kwa Watu wa Mungu, kwani badala ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, Askofu atajikuta akiwa amemezwa na malimwengu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali na kuwaombea Maaskofu wao ili waweze kutekeleza dhamana hii nyeti inayojikita katika upendo kwa ndugu zao katika Kristo, ili kweli familia ya Mungu iendelee kushikamana na kumuungama Kristo Mfufuka. Maaskofu wana karama na mapungungu yao ya kibinadamu, kumbe, kwa njia ya sala, wanaweza kuwa imara na thabiti katika maisha na utume wao mintarafu mpango wa Kristo kwa Kanisa lake.

Kila siku Kanisa linasali kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia. Lakini hili halitoshi kwani kuna wakati majina haya yanatajwa kwa mazoea bila uzito wowote ule. Waamini wanapaswa kusali na kuwaombea Maaskofu wao kwa moyo, ili waweze kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu. Waamini wawaombee Maaskofu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo Mfufuka; Maaskofu wachamungu; vyombo na mashuhuda wa huduma ya upendo; Maaskofu wanaowalisha watu kwa mahubiri ya kina yanayosheheni utajiri wa Neno la Mungu, ili waamini waweze kumfahamu na kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.