2016-01-21 16:03:00

Zanzibar hali ni tete! Watu wanataka kung'oana ndefu!


Askofu Titus Joseph Mdoe, Jumapili tarehe 17 Januari 2016 amesimikwa rasmi kuwa ni Askofu wa tatu wa Jimbo Katoliki Mtwara, tukio ambalo lilitanguliwa na Ibada ya Masifu ya Jioni ambamo alikabidhiwa funguo za Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Mtwara. Ibada ya kumsimika Askofu Titus Mdoe imehudhuriwa na viongozi wa Kanisa, Serikali na Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki Mtwara.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza aligusia mahusiano yaliyopo kati ya maisha ya ndoa na dhamana ya Askofu mahalia pamoja na umuhimu wa Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mtwara kuhakikisha kwamba, inatumia karama na mapaji mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii inayowazunguka. Arusi ya Kana ni mfano wa Askofu ambaye ni Bwana arusi na Jimbo ni bibi arusi. Kumbe, kwa namna ya pekee kabisa, Askofu Titus Mdoe anapaswa kulipenda, kulitumikia na kulihangaikia Jimbo lake la Mtwara kwa hali na mali, ili liweze kuwa ni kielelezo cha uaminifu wa Mungu kwa waja wake; wakati wa raha na shida.

Askofu Mdoe katika maisha yake aliwahi kufanya utume Jimboni Mtwara, lakini wakati huo anaweza kulinganishwa na Mnovisi katika maisha ya kitawa, lakini sasa kama Askofu ni Mtawa aliyeweka nadhiri za daima. Katika maisha kuna wakati watu wanatindikiwa divai kama ilivyokuwa kwenye arusi ya Kanisa, kiasi cha Bikira Maria kuamua kuingilia kati! Divai inaweza kuwakilisha: haki, amani na maridhiano; upendo, umoja na mshikamano. Mambo haya yakikosekana au kupungua, hapo patashika nguo kuchanika inaanza kujitokeza. Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Mtwara kamwe, isitoe nafasi kwa Ibilisi kuwavuruga kwa misingi yoyote ile!

Ndani ya Kanisa hakuna “Mtu wa kuja”, “Mnyamahanga” “Kiyasaka” au mgeni, waamini wote ni sehemu ya Familia ya Mungu inayowajibika. Askofu Titus Mdoe kwa sasa ndiye Bwana arusi wa Jimbo Katoliki Mtwara, anapaswa kupewa ushirikiano, umoja na mshikamano, ili aweze kutekeleza wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume.

Askofu Mdoe anatumwa: kufundisha, kutakatifuza, kuongoza, kuonya, kukaripia na kuwaongoza watu wa Mungu ili waweze kufikia utakatifu wa maisha. Askofu Mdoe pale inapobidi, aonye kwa upole na upendo wa kibaba, daima akitambua kwamba, anapaswa kuwa ni mfano na kielelezo cha Baba mwenye huruma na mchungaji mwema, anayejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kwa namna ya pekee kabisa, Askofu mkuu Ruwa’ichi amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuombea: haki, amani na maridhiano Visiwani Zanzibar ambalo ni tunda la ndoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watanzania wasijidanganye hata kidogo kwamba hali ni shwari wakati ambapo Zanzibar kuna moto unaowaka kichini chini kutokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba 2015. Hadi sasa kuna mikutano ya siri kati ya wadau mbali mbali kuhusiana na mkwazo wa kisiasa Zanzibar, lakini hali bado ni tete. Watanzania katika ujumla wao, wasikae kimya wakati ambapo Zanzibar watu wanatishiana kung’oana ndevu. Viongozi wenye dhamana ya kuhakikisha kwamba Zanzibar kuna kuwa na amani, utulivu na maridhiano watekeleze dhamana hii kwa unyofu, ukweli na uwazi bila kuchelewa sana kwani madhara yake yanaweza kuwa ni maafa kwa watu na mali zao.

Kwa upande wake, Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, baada ya kupokea kiapo cha utii kwa viongozi wa Kanisa Jimboni mwake, aliwashukuru wote na kuahidi kwamba, atajitahidi kuwa ni Baba mwema kwa wote. Viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali wamemshukuru na kumpongeza Askofu mstaafu Gabrieli Mmole aliyetumikia Jimbo Katoliki la Mtwara kwa miaka thelatini na moja. Wamemtakia afya njema ya roho na mwili wakati huu anapoanza ukurasa mpya wa maisha yake kama Askofu mstaafu.

Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, amempongeza Askofu Titus Mdoe kwa kuteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mtwara. Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Padilla ameitaka Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mtwara kuonesha upendo, umoja na mshikamano wa dhati na Mchungaji wao mkuu na kamwe wasimtenge kwa vile tu hakuzaliwa kutoka Mtwara.

Kwa njia ya maisha na utume wake, Askofu Mdoe anajifunga bila ya kujibakiza na Jimbo Katoliki Mtwara, hii ndiyo maana ya alama ya pete ya Kiaskofu. Askofu Mdoe ni kiongozi aliyejipambanua kwa maisha na utume wake, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko amemkabidhi Jimbo Katoliki Mtwara, ili aweze kuwangoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimboni humo.

Naye Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahubiri yake kwenye Masifu ya Jioni, Jumamosi, tarehe 16 Januari 2016, alitumia nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kuwapatia wanafamia ya Mungu Jimbo Katoliki Mtwara, zawadi ya Askofu Titus Joseph Mdoe, kuwa Askofu wao wa tatu. Ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko ili kushika nafasi hii kama Baba, Mchungaji, Mwalimu na Mpatanishi. Askofu ni kwa dhamana na wajibu wake kweli anakuwa ni “Jembe” la huruma ya Mungu kwa wote bila ubaguzi. Askofu Mdoe ni matunda ya kazi ya Uinjilishaji.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam aliongoza ujumbe wa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam katika kumsindikiza na hatimaye kushuhudia Askofu Titus Mdoe akisimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara. Jimbo kuu la Dar es Salaam lilionja cheche za huduma za kichungaji zilizotolewa na Askofu Mdoe, tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu hapo Mei, Mosi, 2013. Askofu msaidizi Euzebius Nzigilwa kwa niaba ya Kardinali Pengo aliyoa salam za shukrani za Jimbo kuu la Dar Es Salaam pamoja na kumkabidhi vifaa vya ibada na chombo cha usafiri kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mtwara.

Viongozi wa Serikali Mkoani Mtwara, wamemkaribisha Askofu Titus Mode kwa mikono miwili na kuahidi kumpatia ushirikiano wa dhati katika kutekeleza dhamana na wajibu wake Jimboni Mtwara. Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha uhuru wa kidini na mahusiano mema kati ya waamini wa dini mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya wengi.

Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.