2016-01-21 10:32:00

Madhabahu ni nyumba ya imani, ukarimu na huruma ya Mungu!


Hija za maisha ya kiroho kwenye madhabahu ni kielelezo makini cha ushuhuda wa imani ya Watu wa Mungu, wanaokimbilia maombezi na msaada kutoka kwa Bikira Maria na Watakatifu; nyenzo muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, dhana inayopaswa kuhimizwa na kuendelezwa, ili kuwasaidia waamini kuishi kikamilifu imani yao kwa njia ya Ibada kwa Kristo Mteswa, Njia ya Msalaba au Rozari takatifu ambao ni muhtasari wa Injili.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipowapokea wafanyakazi wanaowahudumia mahujaji pamoja na wakuu wa Madhabahu mbali mbali, siku ya Alhamisi, tarehe 21 Januari 2016 kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kundi hili. Hujaji ni mtu anayejitahidi kuishi tasaufi ya hija katika undani wa historia na maisha yake; katika mwanga na giza linaloyaandama maisha. Kila mtu ndani mwake anayo sala na ombi maalum na mara anapoingia kwenye madhabahu anajisikia kuwa yuko nyumbani; kwani anapokelewa kwa heshima na taadhima; anaeleweka na kuungwa mkono.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, anapenda sana mfano wa Anna, Mama yake Nabii Samueli aliyekuwa na majonzi makubwa moyoni mwake na akawa anasali akimwomba Mwenyezi Mungu amjalie kupata mtoto. Lakini, Kuhani Eli alipomwona midomo yake ikichezacheza akadhani kwamba alikuwa amelewa mvinyo na akataka kumto nje kwa nguvu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Anna ni mfano wa watu wengi ambao wanakwenda kusali kwenye madhabahu, wanaokaza macho yao kwenye Msalaba wa Kristo Mteswa au kwenye Sanamu ya Bikira Maria, huku wakisali na kutokwa machozi ya matumaini ya sala zao kuweza kusikika. Madhabahu ni mahali muafaka pa kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu ili kuonja huruma yake isiyokuwa na kikomo!

Katika fatakari yake, Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee ukarimu unaojikita katika furaha, wema, upendo na uvumilivu. Injili inamwonesha Yesu aliyekuwa anawapokea na kuwakirimia watu huruma na mapendo. Alifanya hivi hususan kwa wagonjwa, wadhambi na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani wote wanaowapokea wadogo wanampokea Yesu na Baba yake wa mbinguni ambaye amemtuma hapa ulimwenguni. Yesu alizungumzia kuhusu ukarimu na kumwilisha maneno yake katika matendo kwa kuwapokea wadhambi kama Mathayo Mtoza ushuru na Zakayo, kwani watu kama hawa ndio waliojisikia ndani mwao kwamba, wanapokelewa na kuthaminiwa na Yesu Kristo, aliyewasaidia kubadili mwelekeo wa maisha yao.

Mtume Paulo alionesha pia ukarimu kwa wote waliokuwa wanamwendea wakati wa siku zake za mwisho hapa mjini Roma. Nyumba yake ambayo kimsingi ilikuwa gereza, palikuwa ni mahali pa kutangazia Injili na kwamba, ukarimu ni chachu ya Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa tabasamu ili kumwonjesha mtu kwamba, anapokelewa na kupendwa. Mara nyingi hujaji anayewasili kwenye madhabahu anakuwa amechoka, mwenye njaa na kiu; mambo ambayo wakati mwingine ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya maisha ya kiroho. Mtu wa namna hii anahitaji kupokelewa: kiroho na  kimwili na kuhudumiwa vyema, ili aweze kujisikia kuwa kweli amefika nyumbani na wala si tena mgeni au mtu wa kuja!

Hujaji anapofika kwenye madhabahu ajisikie kuwa kweli ni mtu aliyekuwa anasubiriwa, anayependwa na kutazamwa kwa jicho la huruma ya Mungu, bila ubaguzi kwani huruma ya Mungu haina mipaka na katika kila undani wa mtu kuna moyo wenye kiu ya kukutana na Mungu. Wahudumu wa mahujaji wanapaswa kuhakikisha kwamba wanawasaidia watu kueleweka na kupendwa, mambo yatakaomfanya kuwa na ari na moyo wa kutaka kurejea tena kufanya hija kwenye madhabahu haya, kama sehemu ya mchakato wa mwendeleo wa hija ya imani katika maisha yake ya kawaida.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukarimu unajionesha kwa namna ya pekee kwa wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho, wanaowajalia waamini kupata huruma ya Mungu. Madhabahu ni nyumba ya huruma, mahali ambapo kila mwamini anakutana na huruma ya Mungu pasi na ubaguzi. Mwamini anayekimbilia huruma ya Mungu anatambua kwamba, kwanza kabisa anapaswa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kupokelewa na Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma, ili kumkirimia utu na heshima ya kuitwa tena mwana mteule wa Mungu. Mapadre wanao toa huduma kwenye madhabahu wanapaswa kuwa kweli na moyo wa huruma, huku wakionesha ile sura ya Baba mwenye huruma.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kuishi kwa imani na furaha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; kwa kutambua kwamba, wanahimizwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawahakikishia wote hawa sala na sadaka yake, kwa njia ya maombezi na tunza kutoka kwa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.