2016-01-21 10:57:00

Changamoto Sudan: Vita, Njaa, Umaskini na Kiu ya Amani ya Kudumu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Januari 2016 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini, ambalo liko hapa mjini Roma kuhudhuria mkutano maalum ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Kabla ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu walipata muda wa faragha wa siku tano kwenda “Jangwani” ili kufunga, kusali na kutafakari kuhusu maisha na utume wa Kanisa huko Sudan ambako, bado kunawaka moto wa vita na misigano ya kijamii.

Baada ya mafungo, Maaskofu wamekuwa na siku tatu za mikutano na viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, ili kupembua kwa kina na mapana matatizo na changamoto zinazoikabili Familia ya Mungu huko Sudan. Kwa sasa anasema Kardinali Fernando Filoni, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Sudan inakabiliwa na changamoto kuu tatu: vita, umaskini na wimbi kubwa la wakimbizi pamoja na wahamiaji.

Kardinali Zuberi Wako, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ndiye aliyeongoza ujumbe wa Maaskofu walipokuwa wanakutana na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, muda mfupi kabla ya kuanza Katekesi yake kwa siku ya Jumatano ambayo imejikita katika umoja wa Kanisa unaopata chimbuko lake katika zawadi ya imani inayofumbatwa kwenye Sakramenti ya Ubatizo.

Askofu mkuu Paulino Lukudu Loro wa Jimbo kuu la Juba katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, mazungumzo yao na Baba Mtakatifu Francisko limekuwa ni tukio la neema na baraka. Amewasikiliza kwa makini, akachukua mambo msingi ambayo anapenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya Familia ya Mungu Sudan. Amesikitishwa na kuguswa sana na mahangaiko ya wananchi wa Sudan kutokana na vita, njaa, umaskini na mipasuko ya kijamii.

Baba Mtakatifu amewapatia ushauri wa kina kuhusiana na masuala haya nyeti na Maaskofu wametumia fursa hii kumwalika Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Sudan, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo, daima wakiwa tayari kuambata huruma ya Mungu. Changamoto kubwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ni kuendelea kushikamana kama walivyo hata baada ya Sudan ya Kusini kujinyakulia uhuru wake, au kutengana na hivyo kuunda Mabaraza mawili ya Maaskofu Katoliki kwa ajili ya Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini.

Kwa sasa kuna majimbo matano ambayo yako wazi kwa muda mrefu, jambo ambalo ni hatari kwa maisha na utume wa Kanisa hasa ukizingatia ukosefu wa amani na utulivu huko Sudan. Hali ya miito ya Kipadre na Kitawa; haya ni kati ya mambo ambayo Maaskofu wamejadili na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu hapa mjini Vatican.

Askofu mkuu Paulino Lukudu Loro anakaza kusema, haki, amani na maridhiano ni kati ya vipaumbele vya kwanza kwa Familia ya Mungu Sudan ya Kusini, kwani vita inaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Vita imekuwa ni kikwazo kikuu cha ustawi na maendeleo ya wanachi wengi wa Sudan ya Kusini. Majimbo yanahitaji kuwa na wachungaji wake wake wakuu ili kuendeleza kazi ya kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu. Changamoto nyingine ni jinsi ya kulitegemeza Kanisa mahalia. Haya ni mambo msingi ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa Sudan.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.