2016-01-20 07:00:00

Pengo kubwa kati ya maskini na matajiri ni matokeo ya uchumi usiojali!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akishiriki katika mkutano wa kimataifa uliokuwa unajadili kuhusu mchakato wa ujenzi wa uchumi shirikishi na endelevu uliofunguliwa tarehe 17 Januari na kufungwa rasmi hapo tarehe 18 Januari 2016 mjini Roma anasema, pengo kati ya matajiri na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi linazidi kuongezeka kila kukicha, hali inayopelekea watu wengi bado kuendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato. Kutokana na changamoto hizi, kuna haja ya kujenga uchumi shirikishi na endelevu unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi.

Kardinali Parolin anasema, kuna haja kwa magwiji wanaoongoza uchumi wa kimataifa kufanya majadiliano ya wanasiasa, ili kuanzisha mchakato wa sera na uchumi  shirikishi na endelevu. Majadiliano kama haya yasaidie kwa namna ya pekee kumwilisha majadiliano haya katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anaziona changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Yote haya ni matokeo ya uchumi usiowajibika wala kuguswa na mahangaiko ya binadamu.

Uchumi unapaswa kujielekeza katika kusaidia kukidhi mahitaji msingi ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini. Hapa kuna umuhimu wa kujenga madaraja ya watu kukutana na kujadiliana kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli sera na mikakati ya kiuchumi ilenge kudumisha mafao ya wengi, mshikamano, huruma na mapendo. Jumuiya ya Kimataifa katika karne ya ishirini na moja imepambana kufa na kupona na baa la umaskini duniani, lakini bado kuna mengi zaidi yanapaswa kutekelezwa ili kuwanasua watu wengi zaidi kutoka katika dimbwi la umaskini.

Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, anakazia mchakato wa kuzalisha na kugawa rasilimali ya dunia katika usawa; kushirikishana teknolojia rafiki katika shughuli za uzalishaji na huduma; ili kweli uchumi uweze kuwashirikisha wengi sanjari na kuwa endelevu. Dhana hii inawezekana ikiwa kama haki jamii itapewa msukumo wa pekee. Itakumbukwa kwamba, haya ni kati ya mambo ambayo yalikaziwa sana na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hotuba yake kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, alipokuwa anawahutubia wajumbe wa Baraza hilo tarehe 25 Septemba 2015.

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa walikumbushwa kwamba,  ajenda ya maendeleo endelevu kwa mwaka 2030 inahitaji kwa namna ya pekee utashi wa kisiasa, utakaohakikisha kwamba, maamuzi yanayofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa yanatekelezeka; matokeo yake yanafanyiwa tathmini, ili kufanya maboresho pale inapobidi, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Hii ni mikakati makini ambayo isaidia kujenga na kuimarisha uchumi shirikishi na endelevu. Ni matumaini ya Kardinali Pietro Parolin kwamba, majadiliano ya kisiasa na kiuchumi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuwahamasisha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutambua changamoto kubwa iliyoko mbele yao ya athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na uchumi baguzi, ili waweze kuzifanyia kazi changamoto hizi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.