2016-01-20 08:29:00

Majadiliano ya kidini hayana mbadala ili kudumisha amani na usalama duniani


Mheshimiwa Padre Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, hivi karibuni ameshiriki katika Jukwaa la kwanza la Wasomi wa Kiarabu, lililofanyika mjini Abu Dhabi na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wasomi kutoka katika nchi za Kiarabu; wengi wao wakiwa ni waamini wa dini ya Kiislam. Jukwaa la wasomi wa Kiarabu pamoja na mambo mengine limepembua kwa kina na mapana kuhusu misimamo mikali ya kiimani na jinsi ya kudhibiti.

Padre Ayuso anasema, majadiliano ya kidini ni muhimu sana na wala hayana mbadala kati ya waamini wa dini mbali mbali ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Majadiliano ni silaha makini katika kupambana na misimamo mikali ya kidini ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao bila kusahau mipasuko ya kisiasa. Misimamo mikali ya kidini kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ni gumzo la vyombo vya habari kitaifa na kimataifa.

Padre Ayuso anasema, ili kukabiliana na changamoto hii ambayo inahatarisha amani, utu, ustawi na heshima ya binadamu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wa dini mbali mbali kujenga utamaduni wa watu kukutana; kuheshimiana, kupendana na kuthamianiana kama ndugu wamoja na kwamba, tofauti zao za kidini na kiimani, zisiwe ni chanzo cha chokochoko na kinzani, bali hazina inayopaswa kukuzwa na kudumisha kwa ajili ya mafao ya wengi. Majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu sehemu mbali mbali za dunia.

Padre Ayuso anakaza kusema, majadiliano ya kidini yanajenga shule ya ubinadamu na hivyo kuwa niĀ  chachu na chombo chau moja, upendo na mshikamano kati ya waamini wa dini mbali mbali wanaoheshimiana na kupendana kama ndugu na marafiki. Misimamo mikali ya kidini ni kati ya mambo yanayoendelea kuhataarisha amani na usalama sehemu mbali mbali za dunia. Hapa waamini wanapaswa kutambua na kukiri kwamba, misimamo mikali ya kidini na kiimani ni mambo ambayo ni kinyume kabisa cha tunu msingi za maisha ya kidini, kumbe, haina budi kutokomezwa kwa njia ya elimu makini na majadiliano ya kidini ambayo hayana budi kusimamiwa na kuratibiwa na viongozi wa kidini.

Kamwe, viongozi wa kidini wasikubali watu wenye misimamo mikali ya kiimani kuvura amani na mafungamano ya kijamii kwa mgongo wa siasa. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitunza na kuiendeleza. Hii ni dhamana ya kila mtu kuhakikisha kwamba, amani inakuzwa na kudumishwa na wote. Ili kufutilia mbali misimamo mikali ya kidini na kiimani kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kutambua kwamba, dunia itaendelea kukosa amani, ikiwa kama majadiliano ya kidini yatakwama kwa sababu yoyote ile.

Ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujikita katika maisha ya sala kwani sala ni hazina muhimu sana ya maisha ya kiroho, inayomwezesha mwamini kujiaminisha mbele ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Waamini wa dini mbali mbali wachote kwenye hazina ya maisha yao ya kiroho na kimwili hazina na utajiri wa maisha ya sala inayowaunganisha walimwengu wote katika shida na mahangaiko yao, katika haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.