2016-01-20 07:44:00

Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa: Uinjilishaji wa kina!


Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Yangon nchini Myanmar, ambaye ni mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa nchini Ufilippini, litakaloanza kutimua vumbi hapo tarehe 24 hadi 31 Januari 2016 Jimbo kuu la Cebu anasema, mchakato wa Uinjilishaji mpya hauna budi kujikita katika majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali; majadiliano ya kitamaduni, ili kukoleza utamadunisho na kwamba, Kanisa halina budi kuendeleza majadiliano ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maadhimisho ya Kongamano hili yanaongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu”. Kanisa Barani Asia linakabiliwa na changamoto nyingi, zinazopaswa kufanyiwa kazi, lakini kwa kujikita katika majadiliano ya kidini kwani hapa kuna dini nyingi ambazo waamini wake wanabeba ndani mwao utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, ambayo yakitumiwa na wengi, yanaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa msingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Utajiri na hazina ya maisha ya kiroho ni udongo muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Kardinali Charles Maung Bo anakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa, iwe ni fursa kwa Wakatoliki kujenga na kukuza ndani mwao ari na moyo wa huruma. Kila wakati wanaposhiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, watambue kwamba, Ekaristi ni chanzo na kielelezo cha maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Fumbo la Ekaristi Takatifu liwasaidie waamini kujimega na kujitoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao, kwa njia hii, Ekaristi inapata mwelekeo wa kijamii.

Kardinali Charles Maung Bo anafafanua zaidi kwamba, wajumbe wa Kongamano la Ekaristi Takatifu kimataifa nchini Ufilippini wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa dhati ili kuweka sera na mikakati ya pamoja itakayosaidia kupambana na hatari ya kuongezeka na kupanuka kwa ukosefu wa haki msingi katika masuala ya kiuchumi pamoja na uharibifu wa mazingira, changamoto kubwa Barani Asia, inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe, mambo makuu ya kuzingatia ni majadiliano ya kidini, kitamaduni na maskini, ili waweze kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi.

Kardinali Charles Maung Bo anaelezea kwamba, Bara la Asia lina utajiri na hazina kubwa ya maisha ya kidini yanayofumbatwa katika dini mbali mbali; kumbe, utajiri huu uwasaidie wananchi kuheshimiana, kupendana na kusaidiana kwa hali na mali badala ya dini kuwa ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii. Dini ziwe ni chanzo cha haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Bara la Asia lina utajiri mkubwa wa tamaduni zinazoweza pia kusaidia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Tamaduni hizi zikiinjilishwa barabara ni udongo mzuri wa kuweza kupokea Habari Njema ya Wokovu, tayari kuwashirikiana na waamini wa dini mbali mbali. Majadiliano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni muhimu sana kwani hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Kuna idadi kubwa ya maskini Barani Asia, kiasi kwamba, umaskini unaokena kuwa kama dini ya baadhi ya watu. Matokeo yake ni: vita, nyanyaso na dhuluma; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo na idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Umaskini unaendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Charles Maung Bo anawaalika Wakatoliki kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vya maisha yao, sanjari na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, ili kujichotea nguvu ya kuweza kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Waamini wawe mstari wa mbele katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ushuhuda wa Injili ya huruma na mapendo; haki na amani na upatanisho. Kimsingi, Wakristo wanaalikwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.