2016-01-18 15:47:00

Watawa wa Utawa wa tatu wanapania kuyatakatifuza malimwengu


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Karibu tuendelee kuyapamba maadhimisho ya mwaka wa Watawa Duniani, kwa kuendelea kutazama tunu ambazo wapendwa watawa wanatushirikisha sisi waamini ndani ya Kanisa. Baada ya kuzitazama tunu mbalimbali za kiroho na za kimwili ambazo sisi waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema tunaweza kuziiga, leo tuvuke ng’ambo zaidi, tutazame jinsi ambavyo sisi waamini walei pia tunaweza kushiriki Roho na Karama ya mashirika mbalimbali ya kitawa. Lengo la juu kabisa la kushiriki karama za mashirika mbalimbali, ni kukuza au kuchochea zaidi jitihada zetu za kumtafuta, kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu katika mazingira yetu ya kila siku, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Familia ya kitawa katika Shirika lolote lile ni nadharia pan asana. Wapo wanashirika ambao hupokewa na huweka nadhiri, ahadi au vifungo maalumu kadiri ya asili ya shirika husika na katiba yao. Sehemu ya pili, wapo waamini wanaoshiriki karama za mashirika mbalimbali, bila wao wenyewe kuwa watawa katika maana halisi na pasipo ulazima wa kuishi katika jumuiya. Lakini wao nao hufanya utume kama wafanyavyo watawa wenyewe husika katika shirika fulani. Hapo ndipo penye mwanya wa pekee kwa sisi waamini kuyakuza maisha yetu ya Kikrsto kwa msaada wa karama za Shirika fulani la kitawa. Aina hii ya washiriki, kwa lugha ya jumla kabisa huitwa utawa wa tatu, au wale wale washiriki katika Roho na karama ya Mtakatifu Benedikto, huitwa Waoblati.

Kwa siku ya leo mpendwa Msikilizaji tuutazame utawa huo wa tatu wa Mtakatifu Benedikto. Ni akina nani hao? Waoblati wa Mt. Benedikto ni waamini walei waliojitolea kwa Kristo kwa njia ya Mama Bikira Maria ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa kushiriki roho na karama ya Mt. Benedikto. Ni kwa njia hiyo wao wenyewe wanayakamilisha zaidi na zaidi maisha yao ya Kikristo kwa kujibidisha kuziishi fadhili wakiongozwa na Injili Takatifu. Na pia wanasaidia kuchochea na kutunza imani ya Kanisa nyakati zote; na  wanashiriki katika kulitumikia Kanisa kwa moyo wote; na wanajibidisha kutetea na kulinda imani ya kanisa dhidi ya mashambulizi ya adui wa aina mbalimbali. Hawa hawajitengi na maisha ya kawaida. Huishi na hufanya kazi kati ya watu pamoja na wengine katika familia, Jumuiya za watu na katika medani mbali mbali za maisha.

Nani anafaa kuwa Mwoblati? Ni mwamini yoyote yule mbatizwa, mwenye mshikamano na Kanisa Katoliki; na mwenye mwenendo mwema wa Kikristo kadiri ya imani yetu ya kweli Katoliki. Na awe mfuasi wa Kristo kwa maneno na matendo, hadharani na kifichoni. Waliooa au kuolewa, wasiooa wala kuolewa, wajane na wagane, wafanya kazi halali wa kada na ngazi yoyote ile; wote wanaweza kuwa waoblati wa Mtakatifu Benedikto.

Jukumu lao kubwa ni kuiishi roho na karama ya Mtakatifu Benedikto na kuimwilisha tasaufi ya Mtakatifu Benedikto kama inavyojidhihirisha katika Kanuni yake kwa wamonaki. Jitihada kubwa ya Mwoblati ni kuwa mtu wa mfano mwema wa maneno na matendo nyakati zote huku akiongozwa na Neno la Mungu, Mafundisho ya Kanisa, Kanuni ya Mt. Baba yetu Benedikto  na Mifano mbalimbali ya wachaji wa zamani.

Baada ya kipindi cha malezi ya mwanzo, muoblati kwa ibada maalumu huweka ahadi zake kwa Mungu, zikianzia na kipindi cha unovisi na baadaye ahadi za maisha. Kwa vile mwoblati anajitoa mwenyewe ili aweze kuyatakatifuza malimwengu; basi ana wajibu wa daima wa kushika imani ya kweli; kuwa mtu wa sala; tena sala kunjufu, kuwa mchaji wa Mungu kwa ndani na nje, kujifunza tunu mbalimbali za imani; kusoma maandiko matakatifu na kuwa mstari wa mbele katika shughuli za kujitolea kulihudumia Kanisa na watu wote, kuwa mtu wa  kupenda na kujituma kufanya kazi halali ili kuitikia ule wito wa kuutiisha ulimwengu, kupenda kufanya kazi ili kuyakidhi mahitaji ya maisha yake na pia kuwategemeza wahitaji na hivyo kwa njia ya kazi hiyohiyo kujijengea heshima yeye mwenye na kukuza roho za watu. Na zaidi sana, kwa njia ya kazi, mwoblati anashiriki katika kuufundisha na kuurithisha ulimwengu utamaduni wa kazi; anaufundisha ulimwengu Injili ya kazi, na anahamasisha watu wafanye kazi, si kwa maneno tu, bali kwa mfano wa maisha yake mwenyewe.

Waoblati wa Mtakatifu Benedikto daima hujishikamanisha na Monasteri au Abasia maalumu hivyo waweze kuwa chini ya abate fulani mwenye kupokea ahadi zao kwa jina la Kanisa, na waweze kupatiwa misaada mbalimbali ya kiroho. Ni mwaliko kwako mpenda msikilizaji, kutafuta na kuchuchumilia fursa hizi tunazopewa na Mama Kanisa kwa ajili ya kujiimarisha zaidi katika maisha ya Kikristo. Kwa habari zaidi juu ya Uoblati, watafute watawa Wabenediktini popote karibu nawe, uelekezwe na ukiguswa moyo, ujiunge nao, ili sote tulitukuze jina la Bwana pamoja.

Katika kipindi kijacho tutasikia juu ya utawa wa Tatu wa Mtakatifu Fransisko na Mtakatifu Dominiko. Kukuletea makala hii kutoka katika Studio za Radio Vatikan ni mimi Pd. Pambo Matrin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.