2016-01-18 10:56:00

Wakristo ni uzao mteule, ukuhani wa kifalme na taifa la Mungu!


Hija ya kiekumene ni utambulisho muhimu sana miongoni mwa Wakristo, unaowasukuma kutoa ushuhuda wao imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, msingi wa umoja wa Wakristo. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoyatoa Jumatatu tarehe 18 Januari 2016 wakati alipokutana na kuzungumza na waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kutoka Finland ambao kwa sasa wako mjini Roma kwa ajili ya hija ya kiekumene na kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Enric.

Makanisa haya mawili yanaendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene katika taalimungu kwa kuongozwa na Tamko la pamoja juu ya “kuhesabiwa haki katika maisha ya Kanisa” msingi muhimu katika kutafsiri uelewa wa pamoja mintarafu Sakramenti za Kanisa: Kanisa, Ekaristi Takatifu na Utume. Hatua mbali mbali ambazo zimefikiwa kati ya Makanisa haya mawili ni msingi imara wa imani na maisha ya kiroho pamoja na mchakato wa ujenzi na ushirikiano wa kidugu katika hali ya utulivu na maelewano.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini hawa kwamba, Juma la kuombea Umoja wa Wakristo linaloongozwa na kauli mbiu zitangazeni fadhili za Mungu, linawakumbusha Wakristo wote kuwa wao ni uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, ili wapate kuzitangaza fadhili za Mungu aliyewaita kutoka gizani ili waweze kuingia katika nuru yake ya ajabu. Hadi sasa majadiliano ya kiekumene yanaendelea kujikita katika Mafundisho tanzu ya Kanisa na utekelezaji wake, lakini hiki kisiwe ni kizuizi cha hija ya pamoja kuelekea katika umoja wa Wakristo kwa kuvuka vizingiti vya zamani, ambavyo vilisababisha kinzani na mipasuko ya kidini pamoja na hali ya kutothaminiana.

Kwa sasa Wakristo wote wanahamasishwa kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kwa njia ya umoja wa Wakristo, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza Wakristo wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Finland kwa kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira pamoja na ukarimu wao kwake kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Finland. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hija hii ya kiekumene itasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya Jumuiya mbali mbali za Kikristo na hivyo anawatakia wote neema na baraka zake za kidugu. Wote kwa pamoja wamehitimisha mkutano huu kwa kusali Sala ya Baba Yetu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.