2016-01-18 07:47:00

Papa Francisko atembelea Hekalu kuu la Wayahudi Roma


Kanisa Katoliki litaendelea kudumisha majadiliano ya kidini aa Waamini wa dini ya Kiyahudi, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi. Kanisa litaendelea kushirikiana na waamini wa dini ya Kiyahudi ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo sanjari na kudumisha misingi ya haki, amani na ushirikiano na kamwe dini zisiwe ni chanzo cha kinzani na maafa kwa watu na mali zao.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 17 Januari 2016 wakati alipotembelea Hekalu kuu la Waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa tatu kutembelea Hekalu kuu la Kiyahudu mjini Roma: Papa wa kwa kwanza alikuwa ni Mtakatifu Yohane Paulo II na baadaye Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Baba Mtakatifu Francisko anasema, majadiliano ya kidini yamekuwa kwake ni sehemu ya maisha na utume; mambo ambayo yamemsaidia kujenga na kudumisha urafiki na ushirikiano; kwani Wakristo na Wayahudi wanayo mambo mengi yanayowaunganisha pamoja hivyo wanapaswa kujisikia kuwa ni ndugu wamoja. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanao utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa na waamini wa pande hizi mbili.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Wayahudi na Wakristo ni ndugu katika imani na wanaunda familia ya Mungu ambaye anawasindikiza na kuwalinda watu wake. Kama waamini wote kwa pamoja wanahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa Jiji la Roma, kila upande ukijitahidi kuchangia hasa zaidi katika tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kutoa jibu makini kwa changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu. Ni matumaini ya Kanisa Katoliki kwamba, majadiliano ya kidini yataendelea kukuzwa na kudumishwa; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Ili kukoleza majadiliano ya kidini, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameamua kuwatembelea tarehe 17 Januari 2016 Siku ya Majadiliano ya Kidini kati ya Wakatoliki na Wayahudi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi karibuni, Kanisa Katoliki limeadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipotoa Tamko kuhusu majadiliano ya kidini, Nostra aetate; fursa makini ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani aliyewezesha kuwepo kwa mabadiliko ya mahusiano kati ya waamini wa dini hizi mbili. Hali ya kutojaliana imetoweka na sasa waamini wa dini hizi mbili wanashirikiana. Hali ya kuangaliana kama maadui imefutika na kwa sasa waamini wanajisikia kuwa ni marafiki na ndugu wenye asili na urithi mmoja wa maisha ya kiroho.

Kwa mara ya kwanza katika historia, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walifafanua na kubainisha uhusiano kati ya Wakristo na Wayahudi, ingawa hawakuweza kutatua changamoto za kitaalimungu zilizopo, lakini imekuwa ni fursa ya kujenga majadiliano kwa siku za usoni. Kunako tarehe 10 Desemba 2015, Tume ya Kipapa ya mahusiano na Wayahudi imechapisha Waraka mpya unaojishughulisha na majadiliano ya kitaalimungu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni tangu kuchapishwa kwa Tamko la Majadiliano ya kidini na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuhimiza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakatoliki na Wayahudi, huku wakijikita katika mang’amuzi na udumifu, kwani Wayahudi na Wakatoliki wanayo mambo mengi yanayowaunganisha. Hata kama Kanisa linaungama kuhusu wokovu ulioletwa kwa njia ya imani kwa Yesu Kristo, lakini pia linatambua uwepo wa Agano la Kale; upendo endelevu wa Mwenyezi Mungu na uaminifu wake kwa Israeli.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa dini ya Kiyahudi kushirikiana na Kanisa katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo, hususan katika utunzaji bora wa mazingira. Kuna kinzani, vita, mauaji na ukosefu wa haki msingi za binadamu; mambo ambayo yanaacha madonda makubwa katika maisha ya binadamu; mambo ambayo kimsingi yanapingana na mafundisho ya dini zinazoungama imani kwa Mungu mmoja. Maisha ni matakatifu na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Amri ya tano ya Mungu inakataza kuua, kwani Mungu ni asili ya maisha, changamoto kwa waamini kusimama kidete ili kulinda na kudumisha uhai wa mwanadamu. Kila mwanadamu analindwa na kuongozwa na mkono wa huruma ya Mungu, hususan watu wenye shida zaidi. Hawa ni maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, Mungu ni upendo na chemchemi ya uhai, kumbe, mauaji au kifo havina sauti ya mwisho. Waamini wanapaswa kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kumwilisha mantiki ya amani, upatanisho, msamaha na maisha sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, katika historia, Wayahudi wamekumbana na nyanyaso pamoja na dhuluma, kiasi hata cha kukumbana na mauaji ya kimbari wakati wa Shoah. Waamini millioni sita walipoteza maisha yao kwa vile tu walikuwa ni Wayahudi. Haya ni matokeo ya sera zilizotaka mwanadamu kuchukua nafasi ya Mungu. Tarehe 16 Oktoba 1943 zaidi ya waamini elfu moja walipelekwa uhamishoni kutoka Roma kwenda kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz.

Wote hawa wamekumbukwa na Baba Mtakatifu wakati wa hija yake kwenye Hekalu kuu la waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma. Historia iliyopita isaidie kuboresha hali ya siku za usoni; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu wa mwanadamu sanjari na amani. Baba Mtakatifu amewakumbuka wahanga wa Shoah ambao bado wako hai hadi wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa yale yote aliyowawezesha kufanya katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, kwani maelewano, umoja, udugu na urafiki vimekuwa zaidi. Amekumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu amewawekea mbele yao wokovu, kumbe wanapaswa kuwa ni watu wa matumaini. Baba Mtakatifu amewapatia wote baraka na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.