2016-01-18 08:45:00

Lampedusa ni Lango la Huruma ya Mungu na Matumaini kwa wakimbizi!


Kardinali Francesco Montenegro, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Agrigento, Italia, Jumamosi, tarehe 16 Januari 2016 amefungua Lango la Huruma ya Mungu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa “Porto Salvo”, eneo la Lampedusa, alama ya matumaini na maisha mapya kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi Barani Ulaya. Tukio hili limefanyika katika mkesha wa maadhimisho ya Siku ya 102 ya Wakimbizi na Wahamiaji ambayo katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni Jubilei ya wakimbizi na wahamiaji.

Kardinali Montenegro ameamua kwamba, Madhabahu haya ya Bikira Maria, yawe ni mahali muafaka pa kusali na kutafakati kuhusu Injili ya huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; tayari kuimwilisha katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Wakimbizi na wahamiaji wanaendelea kuuliza maswali msingi, ambayo majibu yake anasema Baba Mtakatifu Francisko yanapatikana katika Injili ya huruma ya Mungu. Kardinali Montenegro ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kukabidhi Msalaba aliopewa zawadi na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Cuba. Itakumbukwa kwamba, hii ni zawadi ambayo Baba Mtakatifu Francisko alipewa na Rais Raul Castro wa Cuba.

Lampedusa umekuwa ni mji wa matumaini kwa wakimbizi na wahamiaji wengi wanaokimbia vita, maafa, nyanyaso na madhulumu ya kidini, ingawa wengi wao wanakufa maji hata kabla ya kuwasili kwenye Kisiwa cha Lampedusa. Kwenye Madhabahu ya Bikira Maria kuna maeneo ambayo waamini wa dini mbali mbali wanayatumia kwa ajili kusali. Kumbe Lampedusa ni Lango la huruma ya Mungu kwa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta kuona ushuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu katika maisha yao.

Kardinali Francesco Montenegro anawashukuru waamini na wakazi wa Lampedusa kwa moyo wao wa ukarimu na upendo unaojikita katika Injili ya huruma ya Mungu. Anawahimiza watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ari na moyo mkuu. Lampedusa ni kitovu cha ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi wengi kutoka Barani Afrika, hapa waamini kwa namna ya pekee wajisikie kwamba, wanasukumwa kuonesha ushuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu.

Lango la huruma ya Mungu Lampedusa ni changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Ulaya kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao, kuliko mwelekeo wa sasa wa kutaka kuwafungia mlango wa matumaini ya maisha mapya. Jumuiya ya Ulaya ioneshe sera ya ukarimu, kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi wanaolazimika kukimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali.

Kardinali Montenegro anasema kutokana na maafa makubwa pamoja na mateso wanayokabiliana nayo wakimbizi na wahamiaji, maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kwao imekuwa ni siku ya ukimya na tafakari ya kina, mahali hapa ambapo wakimbizi na wahamiaji wanapita ili kuona mwanga mpya wa maisha yao. Lampedusa ni ufunguo wa matumaini mapya. Baba Mtakatifu Francisko anaguswa kwa namna ya pekee na mahangiko ya wakimbizi na wahamiaji, ndiyo maana hija yake ya kwanza nje ya Vatican ilikuwa ni Kisiwani Lampedusa.

Msalaba uliotolewa kama zawadi na Baba Mtakatifu ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hapa kila mtu anaitwa kusikiliza kilio cha wakimbizi na wahamiaji, ili hata wao waweze kuona mwanga mpya wa Ufufuko wa Kristo baada ya kutembea katika mateso ya Ijumaa kuu. Yesu Kristo ndiye anayemwongoza mwanadamu kuelekea katika Pasaka na maisha mapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.