2016-01-18 08:57:00

Juma la kuombea Umoja wa Wakristo


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Wakristo wote wakati huu wa Juma la kuombea Umoja wa Wakristo wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatangaza fadhili za Mungu katika maisha yao, huku wakiendelea kuambata huruma na upendo wa Mungu. Changamoto hii imekuja kwa wakati muafaka, Kanisa Katoliki linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa Wakristo wote kutafakari kwa kina huruma ya Mungu ambayo kimsingi ni kiini cha imani ya Kikristo.

Majadiliano ya kiekumene pamoja na mambo mengine yasaidie kuimarisha tunu msingi za imani ya Kikristo inayowaunganisha Wakristo wote, badala ya kuendelea kukazia mambo yanayowagawa. Kumbe, Mwaka wa huruma ya Mungu ni nafasi muhimu sana kwa Wakristo kutafakari kiini cha imani yao na hatimaye, kumwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, na huu ndio mchakato wa kuwatangazia watu wa maisha matendo makuu ya Mungu.

Mwaka 2016 ni mwaka wa neema kwani Kanisa la Kiinjili la Kiluteri linajiandaa pia kuadhimisha miaka 500 ya Mageuzi ndani ya Kanisa yaliyofanywa na Martin Luther. Kanisa Katoliki pamoja na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani wamechapisha Waraka wa pamoja unaojulikana kama “ Kutoka kwenye kinzani kuelekea Umoja”. Lengo ni kuonesha nia ya kutaka kuadhimisha kwa pamoja tukio hili la kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa. Kamati maalum inaendelea kubainisha mambo msingi yanayoweza kuingizwa kwenye Ibada ya pamoja, ili kuweza kuadhimisha tukio hili.

Baraza la Kipapa la uhamasishaji a Umoja wa Wakristo linaendelea na maandalizi ya mkutano mkuu utakaowakutanisha Wakatoliki na Waluteri, mwezi Oktoba, mjini Lund, nchini Uswiss, mahali ambapo palizaliwa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani. Wakatoliki na Waluteri, watawaalika wawakilishi wa Makanisa na Madhehebu mengine ya Kikristo ili kushiriki na kutafakari kwa pamoja mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Makanisa,kuelekea katika umoja kamili wa Kanisa.

Mageuzi yaliyofanywa na Martin Luther ndani ya Kanisa anasema Kardinali Kurt Koch ni tukio nyeti ambalo liliwawezesha Wakristo kutambua umuhimu wa Biblia katika maisha yao; Mafundisho kuhusu kukombolewa. Lakini pia Mageuzi haya yameleta utengano ndani ya Kanisa pamoja na vita vya kidini vilivyojitokeza kwenye karne ya kumi na sita na kumi na saba. Leo hii Kanisa linapoona vita ya kidini inayofanywa na waamini wa dini nyingine duniani, Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Wakristo kwamba, hata Wakatoliki na Waluteri, kuna wakati walipigana na kuuana bila huruma.

Kanisa Katoliki linaadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ndani ya Kanisa sanjari na Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican walipoanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hiki ni kipindi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu ambayo ameyawezesha Makanisa mbali mbali kufikia katika maisha na utume wake. Matukio yote haya yawawezesha Wakristo kuwa na matumaini mapya kwa siku za usoni.

Kardinali Kurt Koch anaendelea kufafanua kwamba, Mwaka 2016 Makanisa ya Kiorthodox yanatarajiwa kufanya Sinodi maalum itakayoyaunganisha, tukio ambalo litakuwa ni la kihistoria kabisa. Kanisa la Kiorthodox linajikita kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Sinodi, ili kujenga na kuimarisha umoja kati ya Makanisa haya, ili hatimaye, kusaidia mchakato wa majadiliano ya kitaalimungu, tayari kuelekea katika umoja kamili. Ni matuamini ya Kanisa Katoliki kwamba, Sinodi hii itakuwa ni Pentekoste mpya katika maisha na utume wa Kanisa.

Ubatizo mmoja kwa mandole ya dhambi ni kati ya mada zitakazojadiliwa a wajumbe wa kutoka Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox katika mkutano unaotarajiwa kufanyika mjini Cairo, Misri, mwanzoni mwa mwezi Februari 2016. Mada hii ni nyeti kwani hadi leo hii kuna Makanisa ya Kiorthodox yanawabatiza hata wale Wakristo waliokwisha kubatizwa. Sakramenti ya Ubatizo ni kiini cha majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa. Ni matumaini ya Kardinali Kurt Koch kwamba, Makanisa yataweza kufikia muafaka kuhusu umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.