2016-01-18 08:32:00

Jubilei ya wakimbizi na wahamiaji: katika nyuso zao kuna huruma ya Mungu!


Wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, baada ya kushiriki katika tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Siku ya 102 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, ambayo kwa mwaka huu imeadhimishwa hapo tarehe 17 Januari 2016 wamehudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Ibada hii imeongozwa na Kardinali Antonio Maria Veglio’, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Katika Ibada hii, Msalaba wa Lampedusa ulikuwepo kielelezo cha Injili ya huruma ya Mungu kwa watu zaidi ya elfu nne na kati yao watoto ni takribani mia saba na hamsini waliofariki dunia wakiwa njiani kuelekea Barani Ulaya ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Licha ya idadi kubwa ya watu kuendelea kupoteza maisha wakiwa njiani kuelekea Barani Ulaya, nchini nyingi za Ulaya zimeanza kufunga mipaka yao kwa wakimbizi.

Kumbe, maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wakimbizi, ni tukio la imani na matumaini kwa wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, wasikate tamaa, bali waendelee kutumaini huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wajitahidi kumwilisha imani yao katika matendo ya huruma, kama kielelezo cha ushuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini na wote wanaoteseka kiroho na kimwili!

Askofu Guerino Di Tora, Rais wa Tume na Mfuko wa Wakimbizi Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, ndiye aliyewakaribisha wakimbizi  na wahamiaji waliokuwa kwenye Lango la huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Amesema, wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaonyanyaswa, kudhulumiwa na kuteseka, kumbe huruma ya Mungu ni mwanga ambao wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuonjeshwa katika maisha yao kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Antonio Maria Veglio’ katika mahubiri yake amegusia jinsi ambavyo huruma ya Mungu inavyokuwa ni mafuta ya faraja na tiba inayoganga na kuponya madonda na machungu ya maisha ya wakimbizi na wahamiaji, wanaolazimishwa kukimbia na kuzihama nchi zao kutokana na sababu mbali mbali. Maadhimisho haya yamefanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kielelezo makini cha imani, matumaini, mapendo, udugu na umoja wa Familia ya Mungu inayoundwa na watu kutoka katika makabila, lugha na jamaa mbali mbali.

Kardinali Antinio Maria Veglio’ amemshukuru Mungu kwa zawadi ya imani pamoja na kuendelea kuwakumbuka wale wote wanaokufa maji na baridi wakiwa na tumaini la kufika katika maeneo salama. Wahamiaji na wakimbizi ni changamoto kubwa na endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi nawadau mbali mbali, kwa kujikita katika kukuza na kudimisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Nyuso za wakimbizi na wahamiaji zinaonesha historia ya matukio mbali mbali ya maisha; watu ambao wanateseka na kukataliwa; watu wenye wasi wasi na mashaka na maisha yao; lakini pia ni nyuso za matumaini kwa usalama na maisha bora zaidi.

Uwepo wa wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa la kiulimwengu na Makanisa mahalia unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani, tamaduni, ibada na Mapokeo ya Kanisa. Wakimbizi na wahamiaji wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanashirikisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu kwa Jamii zinaowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha.

Kamwe wakimbizi na wahamiaji wasibeze imani, tamaduni, mila na desturi njema kutoka katika nchi zao. Watambue na kuthamini karama na vipaji mbali mbali ambavyo Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha, pale inapowezekana, wavifanyie kazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao binafsi, jamii na Kanisa katika ujumla wake.

Wakimbizi na wahamiaji walioshiriki Ibada hii ya Misa Takatifu wamemshukuru Mungu kwa kuwapatia fursa ya kusali, kutafakari na kukutana na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaounganishwa na imani moja kwa Kristo na Kanisa lake. Imekuwa ni fursa ya kusaidiana na kutiana shime katika shida na magumu ya maisha, pasi na kukata tamaa. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; mwaliko wa kumwilisha huruma, upendo na mshikamano.

Wakimbizi na wahamiaji hawa wanasema Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kusamehe na kusahau, tayari kuanza ukurasa mpya unaoandikwa kwa lugha ya huruma ya Mungu kwa waja wake. Wakimbizi na wahamiaji wanasema, haki, amani, msamaha na upatanisho wa kweli unaweza kuvunjilia mbali chuki na uhasama; vita na mipasuko ya kijamii inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha  ya watu na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.