2016-01-18 16:22:00

Amani na usalama; huduma kwa wakimbizi yamejadiliwa na Papa na Mfalme Albert II


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 18 Januari 2016 amekutana na kuzungumza na Mfalme Albert II kutoka Monaco aliyekuwa ameambatana na mkewe Malkia Charlene; ambao baadaye wamekutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na wageni wake, wamefurahishwa na mahusiano mema yaliyopo kati ya nchi hizi mbili, lakini kwa namna ya pekee wamepongeza mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Monaco. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wamegusia pia masuala kadhaa yanayohusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; msaada wa kibinadamu sanjari na mchakato wa maendeleo endelevu yanayogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mwishoni, Baba Mtakatifu pamoja na wageni wake wamegusia kwa namna ya pekee kabisa masuala nyeti yanayoendelea kuitikisa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu, hususan suala zima la amani na usalama; ukarimu na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na hali ya jumla huko Mashariki ya Kati na kwenye Ukanda wa Bahari ya Mediterrania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.