2016-01-16 09:25:00

Mwono wa Kiekumene wa Papa Francisko: Upendo, Ukweli, Sala na Damu!


Maadhimisho ya Juma la kuombea umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2016 yanakazia kwa namna ya pekee uhusiano uliopo kati ya Sakramenti ya Ubatizo na Ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo katika medani mbali mbali za maisha kama njia ya kutangaza fadhili za Mungu, kauli mbiu inaoongoza maadhimisho haya tangu tarehe 18 hadi tarehe 25 Januari 2016, Siku kuu ya kuongoza kwa Mtakatifu Paulo, mwalimu na mtume wa mataifa! Itakumbukwa kwamba, sala na tafakari kwa mwaka huu zimeandaliwa na kikundi cha kiekumene kutoka Lithuania.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa linalohamasisha Umoja wa Wakristo anasema kwamba,  maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa majadiliano ya kidini yanajikita katika mambo makuu manne! Mosi ni Uekumene wa upendo unaojikita katika udugu na urafiki; msamaha na upatanisho miongoni mwa Wakristo. Pili ni Uekumene wa ukweli unaoambata majadiliano ya kitaalimungu kwa kushirikishana mang’amuzi na vipaumbele vya maisha na utume wa Makanisa kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Tatu, Uekuemene hauna budi kusimikwa katika umoja wa Wakristo unaoshuhudiwa katika sala ya pamoja; kwa kufanya kazi kwa ushirikiano; kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wakristo watambue kwamba, umoja ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Kristo! Nne, Baba Mtakatifu anazungumzia Uekumene wa damu unaoshuhudiwa na damu ya Wakristo wanaoendelea kuteseka na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia!

Kardinali Koch anafafanua kwamba, tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu ameonesha azma ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene uliozinduliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili Vatican. Hapa kuna haja ya kushirikiana kwa karibu zaidi kwa kuonesha Uekumene wa upendo unaojikita katika udugu na urafiki mambo yanayowasaidia Wakristo kuonana, kusali na kushirikiana kama ndugu.

Hapa Baba Mtakatifu ameendelea kushuhudia msimamo huu kwa kukutana na kutembelea Jumuiya mbali mbali za Kikristo katika kutafuta ukweli unaowakutanisha kama wafuasi wa Kristo. Katika matukio mbali mbali, Baba Mtakatifu ameomba msamaha na upatanisho kwa niaba ya Waamini wa Kanisa Katoliki waliosababisha mateso na nyanyaso kwa wakristo wenzao. Wakristo watambue kwamba, wote wametenda dhambi na wanahitaji kufanya toba na wongofu wa ndani, ili waweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi zao. Waamini watambue udhaifu wao wa kibinadamu, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakazia Uekumene wa ukweli na kwamba, majadiliano ya kitaalimungu ingawa ni muhimu sana, lakini hayana uzito sana kwani Kristo anaweza kurudi kuwahukumu wazima na wafu na hapo atawakuta bado wakijadiliana pasi na kufikia muafaka. Majadiliano ya kitaalimungu yajikite katika imani, matumaini na mapendo, mambo msingi katika sayansi ya Mungu, “Scienza Dei”. Taalimungu ya kiekumene haina budi kujikita katika sala kwa kupiga na kuchubua magoti, ili kumwomba Kristo awakirimie zawadi ya umoja, inayofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Majadiliano ya kiekumene yanapaswa kujikita katika kushirikishana zawadi ambazo Roho Mtakatifu anayakirimia Makanisa haya. Kwa sasa Kanisa Katoliki linaendelea kutafakari kuhusu dhana ya Urika wa Maaskofu na Sinodi kutoka katika Makanisa ya Mashariki, ili dhana hizi ziweze kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki, wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Haya ni majadiliano ya kiekumene yanayoyawezesha Makanisa kusali, kufanya kazi kwa ushirikiano, Kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Huu ni mwaliko wa kushikamana katika mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, haki na amani; uhuru wa kuabudu; pamoja na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kimsingi, Wakristo wanaweza kushirikiana na kushikamana katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni. Kwa njia hii, Wakristo wataendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya Kristo, mchakato unaofumbatwa katika dhana ya Uinjilishaji mpya. Ikumbukwe kwamba, umoja wa Wakristo ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Kristo, linalohamasishwa kujielekeza zaidi katika upatanisho na umoja. Sala ya pamoja ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha Umoja wa Wakristo. Huu anasema Baba Mtakatifu ni Uekumene wa maisha ya kiroho, dhana iliyopewa msukumo wa pekee na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Uekumene wa damu unawaunganisha Wakristo wote wanaoteseka, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa la mwanzo lilikuwa na kushamiri kutokana na damu ya Wakristo, iliyogeuka kuwa ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia. Damu ya mashuhuda wa imani iwe ni mbegu ya umoja wa Wakristo.

Kardinali Kurt Koch anakamilisha tafakari yake ya kina kuhusu mambo makuu manne yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kukaza kwamba, majadiliano ya kiekumene ni dhamana nyeti kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.