2016-01-15 14:53:00

P. Ermes Ronchi kuongoza Mafungo ya kiroho kwa Papa na wasaidizi wake wa karibu


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Ermes Ronchi wa Shirika la “Servi di Maria” kuongoza mafungo ya maisha ya kiroho wakati wa mafungo ya Kwaresima kwa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kumwandaa Baba Mtakatifu mwenyewe pamoja na wasaidizi wake wa karibu ili waweze kuwa kweli ni wamissionari, mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, Kwaresima ya mwaka huu wanaipatia uzito mkubwa zaidi, ili kuonja huruma ya Mungu. Hiki kiwe ni kipindi cha sala, tafakari na kufunga; kwa kuambata Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu kuanzia tarehe 6 Machi hadi tarehe 11 Machi 2016 “watajichimbia” kwenye nyumba ya mafungo ya “Casa del Divin Pastore” iliyoko Ariccia, nje kidogo ya Jiji la Roma. Padre Ermes Ronchi anasema, amepokea simu moja kwa moja kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko akimwomba asaidie kuwaongoza katika mafungo ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu.

Padre Ronchi anasema, alipigwa na mshangao mkubwa si kutokana na dhamana na utume alioombwa kuutekeleza na Baba Mtakatifu, bali jinsi alivyoonesha utu na unyenyekevu wa hali ya juu, kiasi cha kuamsha ari na hamu ya kutaka kukutana na kuonana na Baba Mtakatifu Francisko. Jibu la kwanza lilikuwa ni hapana kwani hajisikii kuwa na uwezo wa kutekeleza dhamana hii kubwa! Baba Mtakatifu akamwomba tena ili kuangalia ikiwa kama katika tarehe alizompangia alikuwa huru kutekeleza dhamana hii.

Padre Ronchi anasema baada ya kukubali mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa sasa ameanza kujiandaa ili kuhakikisha kwamba, anawashirikisha ule utajiri wa Neno la Mungu na mang’amuzi ya maisha yake, ambayo kimsingi yameacha chapa ya kudumu katika wito na maisha yake ya kipadre. Padre Ermes Ronchi anakaza kusema, Maandiko Matakatifu yana utajiri mkubwa unaoonesha Sura ya huruma ya Mungu, ambayo ni Kristo Yesu mwenyewe. Hiki ni kiini, uzuri na nguvu ya Injili.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Injili ya furaha kwa namna ya pekee anawaalika Wakleri kuandaa vyema mahubiri yatakayogusa maisha ya watu, yawe mafupi, lakini muhimu sana. Padre Ronchi anasema, tangu mwanzo wa maisha na utume wake wa Kipadre anapenda kutoa mahubiri mafupi, yanayogusa sakafu ya mioyo ya watu na kuacha chapa ya kudumu, inayopaswa kufanyiwa kazi. Neno la Mungu halina budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha imani tendaji.

Mahubiri yake anaendelea kufafanua ni hija ya maisha na utume wake, ambao wakati mwingine umekuwa ni chemchemi ya furaha; masikito na matumaini ya kusonga mbele kwa imani na matumaini sanjari na kutambua kwamba, kama waamini wanaogelea katika dimbwi la upendo na huruma ya Mungu katika maisha. Mahubiri lazima yawe na mwelekeo chanya, kwa kujikita katika matumaini kwani Injili ni Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amefungua ukurasa mpya kwa maisha na utume wa Kanisa. Amekuwa kweli ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi kwa njia ya maneno, lakini zaidi matendo yake; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utume huu ni matunda ya Roho Mtakatifu, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. .

Padre Ronchi anakaza kusema, katika mahubiri yake, hapana shaka kwamba, Bikira Maria atakuwa na nafasi ya pekee kabisa kwani huyu ni Mama wa huruma na upendo wa Mungu; Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; mwanafunzi wa kwanza kuonja na kushuhudia huruma ya Mungu kwa binadamu. Bikira Mama anayejisadaka bila ya kujibakiza kwenda milimani kumsaidia binamu yake Elizabeth aliyekuwa ni mjamzito, changamoto kwa waamini kumwilisha matendo ya huruma kwa kuonesha mapendo kwa jirani. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwa kweli ni vyombo vya upendo na huruma ya Mungu anayeendelea pia kujimwilisha katika maisha ya watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.