2016-01-15 12:26:00

Jimbo Katoliki Mtwara, Tanzania kumekucha!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anatarajiwa kuongoza msafara wa familia ya Mungu kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam ili kumsindikiza Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara anayetarajiwa kusimikwa rasmi, Jumapili tarehe 17 Januari 2016, akiwa ni Askofu wa tatu kuliongoza Jimbo Katoliki la Mtwara lililoanzishwa kunako tarehe 18 Januari 1973. Jimbo hili limewahi kuongozwa na Hayati Askofu Maurus Libaba na Askofu mstaafu Gabrieli Mmole aliyeliongoza Jimbo la Mtwara kuanzia mwaka 1988 hadi mwaka 2015 alipong’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu Francisko akamteua Askofu Titus Joseph Mdoe kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mtwara.

Taarifa zinaonesha kwamba, Askofu Titus Mdoe Jumamosi jioni anatarajiwa kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni baada ya kukabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu, Jimbo kuu la Mtwara na Jumapili tarehe 17 Januari atasimikwa rasmi kuwa Askofu wa tatu wa Jimbo Katoliki Mtwara katika Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuhudhuriwa na familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Mtwara.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anamshukuru na kumpongeza Askofu mstaafu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki Mtwara aliyejitahidi kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Mtwara, tangu tarehe 25 Mei 1988 alipowekwa wakfu kuwa Askofu hadi mwaka 2015 alipong’atuka kutoka madarakani kutokana na afya yake kuanza kuzorota. Kipindi chote hiki ameliimarisha Kanisa na kwa sasa linasonga mbele.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteua Askofu Titus Joseph Mdoe kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mtwara, baada ya kutoa huduma ya kutukuka Jimbo kuu la Dar es Salaam kama Askofu msaidizi. Maaskofu wenzake wanamwombea heri na baraka katika utume wake huu mpya, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Wanaitaka Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mtwara iwe kweli ni familia inayomwadhimisha, shuhudia na kumhubiri Yesu Kristo kwa njia ya maisha, kielelezo cha imani tendaji.

Askofu Ngalalekumtwa anawakumbusha Wakristo Jimbo Katoliki la Mtwara kuwa ni wachache, kumbe wanapaswa kujikita pia katika majadiliano ya kidini, ilikukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya waamini, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Wakristo waoneshe msimamo wa umoja na Kiongozi wao mkuu, ambaye kwa sasa ni Askofu Titus Joseph Mdoe, ili Kristo Yesu azidi kutangazwa na kushuhudiwa; Mwenyezi Mungu apewe sifa, utukufu, heshima na shukrani; ili familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Mtwara iweze kupata heri, neema na baraka kwa uwepo wa Kanisa katika eneo hili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania liko njiani kuelekea Mtwara, tayari kushiriki katika Ibada ya kumsimika Askofu Titus Joseph Mdoe kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mtwara. Waamini wanahamasishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhakikisha kwamba wanampokea Askofu Mdoe, ili kwa pamoja waweze kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika huruma, upendo, haki, msamaha na unyenyekevu, tayari kumpatia nafasi Kristo aweze kuitawala na kuiongoza akili na mioyo yao ili nao waweze kuyatawala vyema mazingira yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.