2016-01-15 11:14:00

Historia ya taabu na magumu ya maisha, iwe ni chachu ya ukarimu!


Wakimbizi na wahamiaji ni dhana endelevu katika historia ya maisha ya mwanadamu na kwamba,  familia ya binadamu inapaswa kuwa na sera, mikakati na mipango thabiti ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi pamoja na wahamiaji; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea utu, heshima na haki zao msingi, kwa kutambua kwamba, hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wakimbizi na wahamiaji wanaendelea kuuliza maswali mengi katika maisha yao, lakini majibu makini kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko yanapata jibu katika Injili ya huruma ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 102 ya Wakimbizi na Wahamiaji duniani, hapo tarehe 17 Januari 2015. Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaotafuta usalama na ubora wa maisha baada ya kukumbana na vita, maafa, nyanyaso na dhuluma ambazo wakati mwingine zinafanywa kwa misingi ya udini usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Askofu John Buckley wa Jimbo Katoliki la Cork, Ireland anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, wanahamasishwa na Maandiko Matakatifu kuwapokea na kuwakirimia wahamiaji na wakimbizi, wakitambua kwamba, hata wao wakati fulani katika historia walikuwa ni wakimbizi na wahamiaji, wakateseka na kunyanyasika katika ujenzi wa Jiji la London. Walifanyishwa kazi za suluba katika migodi ya madini Yorkshire, wakabebeshwa mizigo kama watumwa kwenye bandari ya Boston, nchini Marekani. Ni watu waliopelekwa mchakamchaka katika ujenzi wa miji kama Sydney na Perth, leo hii ukiiona inavutia kwa macho! Lakini ni miji ambayo imejengwa kwa jasho la wahamiaji na wakimbizi kutoka Ireland. Mtakatifu Patrick, msimamizi wa Ireland alikuwa ni mkimbizi na mtumwa.

Kumbe, wakimbizi na wahamiaji wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya nchi wahisani, ikiwa kama wataheshimiwa na kuthaminiwa, Watapewa haki zao msingi, na utu wao kuendelezwa na kudumishwa na wote. Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2016 iwe ni fursa pia ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Dhana ya wakimbizi na wahamiaji ni changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi kwa jicho la huruma ya Mungu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.