2016-01-14 06:52:00

Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wakimbizi na wahamiaji 2016


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 17 Januari 2016 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, nyakati hizi kuitazama kwa makini sana huruma ya Mungu ili kuona ishara za wazi kabisa za utendaji wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya watu. Upendo wa Mungu unapaswa kuwafikia watu wote na kuwaletea mabadiliko wale wote wanaokumbatia huruma ya Mungu, tayari kuwashirikisha wengine huruma hii, ili kila mwanadamu aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani katika familia moja ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa mchungaji mwema, anayeguswa na mahitaji ya wagonjwa, wachovu, waliojeruhiwa na wote wanaohitaji msaada. Hivi ndivyo Yesu Kristo alivyowahubiriwa watu kuhusu huruma ya Baba, kiasi hata cha kuinama ili kuganga na kuponya umaskini wa binadamu: kiroho, kimwili na kimaadili; pale hali hii inapokuwa mbaya zaidi, hapo huruma ya Mungu inazidi kuongezeka maradufu. Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2016 ni “Wahamiaji na Wakimbizi wanatuuliza. Jibu la Injili ya Huruma”

Baba Mtakatifu anasema, wakimbizi katika nyakati hizi ni changamoto pevu kwani kunaongezeko kubwa la wahamiaji na wakimbizi wanaozikimbia nchi zao, watu hawa wanaacha maswali kwa mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake, kiasi cha kuleta changamoto katika mfumo wa mapokeo ya maisha, kiasi hata wakati mwingine wa kuvuka mwelekeo wa kitamaduni na kijamii katika maeneo wanakoelekea. Mara nyingi hawa ni waathirika wa vita na umaskini; watu wanaokimbia ili kusalimisha maisha yao, lakini wakiwa na ndoto ya maisha bora zaidi njiani wanakumbana na wafanyabiashara ya binadamu; ni watu wanaonyanyasika, kiasi cha kuishi katika woga na wasi wasi. Hata katika nchi zinazotoa hifadhi wanakabiliwa na sheria na taratibu ngumu ambazo wakati mwingine hazitekelezeki, kuna haja ya kuhakikisha kwamba kunakuwepo na utaratibu mzuri wa kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji, tayari kuwaingiza katika mfumo wa jamii husika, kwa kuzingatia haki na wajibu msingi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kadiri muda unavyozidi kuyoyoma ndivyo Injili ya huruma inayotikisa dhamiri za waamini ili kwamba wasifanye mazoea ya mahangaiko na mateso ya wengine na badala yake wawe wepesi kumwilisha fadhila za kimungu yaani: imani, matumaini na mapendo katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hili ndilo jibu makini linalopaswa kububujika kutoka katika Injili ya huruma ya Mungu. Wimbi la wakimbizi na wahamiaji ni ukweli unaopaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuangalia sababu zinazopelekea watu kukimbia au kuhama nchi zao; mabadiliko yanayojitokeza kwa jamii na watu kuona sura mpya. Hii ni changamoto pia kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, inashughulikia kikamilifu kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia, kwani ukimya na hali ya kutojali kunapelekea maafa makubwa kwa watu kupoteza maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaopambana dhidi ya umaskini, njaa, unyonyaji pamoja na ugawaji mbaya wa rasilimali ya dunia ambayo inapaswa kutumiwa vyema na wote. Kila mtu ana hamu ya kutaka kuboresha hali yake ya maisha sanjari na kupata kipato cha haki atakachowashirikisha ndugu zake. Kuna uhamiaji ambao unayafanya baadhi ya makundi ya watu kupoteza utambulisho wao, jambo hili halipaswi kupuuziwa.

Wahamiaji wanajikuta wakati mwingine wakilazimika kubadilika kadiri ya mazingira ya jamii inayowakirimia, kiasi kwamba, wakati mwingine, mambo haya yamekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya kweli, badala ya kuwa ni fursa ya ukuaji wa mtu: kiutu, kijamii na kiroho, kwa kuheshimu tunu msingi zinazompatia mtu utambulisho wake wa haki katika mahusiano na Mwenyezi Mungu; jirani  na mazingira Hii ni changamoto kubwa kwa jamii inayowapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, kwani zinaweza kujikuta zikihangaika kama hakuna utaratibu na mipango thabiti. Matokeo yake ni mchakato wa kuwaingiza wakimbizi na wahamiaji ambao ulipaswa kua ni utajiri mkubwa, unaanza kukabiliwa na vitendo vya kibaguzi, hofu zisizo na msingi pamoja na utaifa.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Maandiko Matakatifu yanawahamasisha waamini kuonesha ukarimu kwa wageni na kwa kufanya hivyo wanamfungulia Mungu malango na katika sura ya jirani, hapo Kristo Yesu anajidhihirisha mwenyewe. Taasisi, vyama vya kitume na mashirika mbali mbali ya kijimbo, kitaifa na kimataifa yanaendelea kupata mang’amuzi ya pekee yanayofumbata furaha ya watu kukutana na kuoneshana mshikamano, wakiwa wanaongozwa na maneno ya Yesu anayesimama mlangoni na kubisha hodi. Ni makundi yanayoendeleza majadiliano kuhusu, hali, haki na changamoto katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kuwa na sera na mikakati bora zaidi. Lakini pia kuna baadhi ya Jumuiya za Kiparokia zinaona kana kwamba, uwepo wa wahamiaji na wakimbizi ni jambo ambalo linahatarisha amani, usalama wao.

Katika mazingira kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko, jibu makini linapatikana katika Injili ya huruma inayomwonesha Yesu Kristo kuwa ni zawadi ambayo ikipokelewa kwa imani na matumaini, inakuwa ni chemchemi ya matumani na shukrani kwa wale wote wanaofumbatwa katika Fumbo la Ukombozi ulioletwa na Kristo Yesu kwa kumwaga Damu yake azizi, changamoto ya kuambata upendo na mshikamano sanjari na kuwajibika katika kulinda, kutetea na kuendeleza ustawi wa wakimbizi na wahamiaji. Hapa watu wajenge utamaduni wa kukutana na wengine katika urafiki kwa kuwa tayari kutoa na kupokea kutoka kwa wengine, kwani huu ndio mwelekeo sahihi wa ukarimu.

Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, kwanza kabisa wao ni binadamu, ambao utu na heshima yao vinapaswa kulindwa na kudumishwa na kwa njia hii, wanaweza kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya wengi, hasa pale wanapotekeleza nyajibu zao kwa Jumuiya inayowapokea na kuwapatia hifadhi, pamoja na kuendelea kuheshimu urithi wa maisha ya kiroho na kimwili kwa nchi wahisani. Wawe makini kuheshimu sheria na taratibu za nchi husika.

Lakini, haiwezekani kabisa kwa wakimbizi na wahamiaji kuangaliwa tu katika misingi ya kisheria, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Haya ni mambo msingi katika mchakato wa kumwendeleza binadamu, kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana ili kudumisha umoja, kwa kusukumwa na Injili ya huruma ambayo inapaswa kuwa kweli ni chachu inayoleta mabadiliko katika maisha ya binadamu. Mama Kanisa anaunga mkono juhudi zote zinazotaka kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa kuwasaidia watu kubaki katika nchi zao, ili kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watu wao. Jambo la msingi ni kuzisaidia nchi wanamotoka wakimbizi na wahamiaji, kwa njia ya mshikamano unaojikita katika kanuni auni, ili kuendeleza ushirikiano wa kimataifa sanjari na ugawanaji sawa wa rasilimali ya dunia.

Haya ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa nchi wanakotoka wakimbizi na wahamiaji, ili kusaidia kuboresha hali ili watu waweze kuona fahari ya kubaki katika mazingira yao ya asili na utamaduni wao. Kuna haja pia ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inadhibiti kikamilifu matukio yote yanayoweza kusababisha watu kukimbia na kuhama nchi zao kama vile: umaskini, vita na madhulumu. Kuhusiana na masuala haya, wananchi wanapaswa kuelimishwa barabara, ili kuondokana na wasi wasi usiokuwa na mashiko pamoja na unyonyaji wanaoweza kufanyiwa wahamiaji na wakimbizi.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba haguswi na nyanyaso pamoja na dhuluma zinazofumbatwa katika utumwa mamboleo unaojikita katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; kazi za suluba na mshahara “kiduchu” kwa watoto na wanawake; watoto kupelekwa mstari wa mbele kama askari na chambo cha vita; baadhi ya watu kulazimishwa kuwa ombaomba mitaani bila kusahau biashara ya ngono!

Haya ni baadhi ya mambo ambayo wakimbizi na wahamiaji wanakabiliana nayo, changamoto kwa Mama Kanisa na Jumuiya binadamu, kuona na kuguswa na ile Sura ya huruma ya Mungu, ili waweze kupata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, asili ya faraja zote. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wahamiaji na wakimbizi ni sehemu ya kiini cha Injili ya huruma ya Mungu inayowahamasisha waamini kujenga utamaduni wa watu kukutana na kuoneshana ukarimu ambao ni kielelezo cha ukarimu kwa Mungu mwenyewe. Waamini kamwe wasikubali kupokonywa matumaini na furaha, chemchemi ya huruma ya Mungu inayoonekana kati ya watu wanaokutana nao kila siku ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi kwa mwaka 2016 kwa kuwaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Familia Takatifu ya Maria na Yosefu iliyolazimika kukimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu wale wote wanaojisadaka kwa hali na mali kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.