2016-01-13 10:51:00

Masista wanne Wakarmeli Tanzania, waweka nadhiri zao za daima huko Boko!


Askofu Titus Mdoe aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mtwara, anatarajiwa Jumapili ijayo, tarehe 17 Januari 2016 kusimikwa rasmi tayari kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza waamini wa Jimbo Katoliki Mtwara. Kabla ya kuondoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu Mdoe, hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya nadhiri za Watawa wanne wa Shirika la Masista Wakarmeli Wamissionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, ibada ambayo imeadhimishwa kwenye Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Sr. Donatella Capello, Mama mkuu wa Shirika ulimwenguni amepokea nadhiri za watawa wake.

Watawa walioweka nadhiri zao za daima walimwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kusikiliza sauti yao na kuwa tayari kuitikia ili kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya Wakfu. Walimshukuru Mungu aliyewaangalia katika unyonge wao na kuamua kuwainua juu kama mlingoti wa bendera, kiasi kwamba, sasa wako tayari kutumwa sehemu mbali mbali za dunia kama vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa hawa wanatambua kwamba, wao ni watumishi wa Bwana na wanapaswa kutenda kadiri ya matashi ya Mungu, kwa njia hii wako tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kadiri ya mwongozo wa Shirika lao!

Askofu Titus Mdoe katika mahubiri yake anakaza kusema, Mwenyezi Mungu anamwita kila mwamini kadiri ya mapenzi yake na kila mwamini anajibu kadiri ya wito wake. Mwitikio wa watawa hawa unaonesha jinsi ambavyo wako tayari kumtumikia Mungu, Kanisa na jirani kwa njia ya Shirika la Masista Wakarmeli Wamissionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Baada ya tafakari na majiundo makini katika maisha na utume wa kitawa, hatimaye, watawa hawa wamefikia uamuzi wa kujisadaka maisha yao yote kwa njia ya Nadhiri za daima.

Askofu Mdoe anaendelea kufafanua kwamba, katika Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanajitwalia dhamana na wajibu unaowashirikisha: ukuhani, unabiii na ufalme wa Kristo; chapa inayodumu maisha yao yote. Imani inayoungamwa, adhimishwa, mwilishwa na kusaliwa na waamini inapaswa kupata chapa ya daima katika maisha ya waamini anasema Askofu Mdoe. Hii inatokana na ukweli kwamba, katika maisha ya mwanadamu, daima kuna mapambano kati ya wema na ubaya. Kumbe, ni wajibu wa waamini kusimama kidete kupinga nguvu za mwovu shetani kwa kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Askofu Mdoe anasema kwamba, Watu wa Mungu wana njia na miito tofauti ya kumtumikia Mungu katika: Maisha ya ndoa na familia; katika wito wa Upadre na maisha ya kitawa. Miito yote hii inaonesha uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake na kwamba, watawa walioweka nadhiri zao, ni changamoto ya Watu wa Mungu kuendelea kumtumikia Mungu kwa moyo na akili zao zote, sasa na daima katika maisha. Nadhiri ya utii, inamwonesha Kristo aliyekuwa mtii katika kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, akazaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kwa njia ya ufukara, Yesu alijinyenyekesha akajitwalia hali ya ubinadamu na kuzaliwa kwake Bikira Maria aliyekuwa Tabernakulo ya kwanza ya huruma ya Mungu.

Na kwa njia ya ufukara wake, anataka kuwafundisha wafuasi wake wote kumtumainia Mungu katika maisha yao ya kila siku. Yesu alionesha usafi kamili, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli watakatifu na wakamilifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni. Kwa njia ya nadhiri ya usafi kamili, watawa wanajisadaka kwa ajili ya Mungu, Kanisa na jirani zao.

Kwa hisani ya Padre Egidio Seneda, C.PP.S.

Dodoma, Tanzania. 








All the contents on this site are copyrighted ©.