2016-01-13 12:15:00

Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kuangalia matukio kwa jicho la huruma!


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican anasema, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuangalia matukio mbali mbali ya kimataifa kwa jicho la huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican amegusia maafa na majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, bila ya kulaani, bali kuwaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujisikia kwamba, wanatiwa shime na ari ya kuweza kukabiliana na changamoto hizi bila ya kukata tamaa, pamoja na kuendelea kushirikiana kwa dhati, mwanadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Vatican inapenda kushirikiana bega kwa bega na Jumuiya ya Kimataifa katika utekelezaji wa misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu anaendelea kukemea kwa moyo wake wote vitendo vya kigaidi vinavyofanywa kwa misingi ya misimamo mikali ya kidini, kwa kuwataka waamini wa dini mbali mbali kushinda kishawishi cha misimamo mikali ya kidini kwa kuambata majadiliano ya kidini yanayojikita katika ukweli na uwazi; kwa kufahamiana na kuheshimiana kwani mauaji ya kinyama kwa kisingizio cha udini ni kashfa kubwa inayoendelea kutikisa dhamiri za watu wengi duniani; kashfa inayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya kimataifa. Dini zinapaswa kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu na wala si kinyume chake.

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema, Baba Mtakatifu amegusia kwa uchungu mkubwa hatima ya wahamiaji na wakimbizi wanaoendelea kupoteza maisha yao kwa sababu mbali mbali. Hawa ni watu wenye utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanapaswa kuheshimiwa, kuhudumiwa na kusaidiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anawapongeza watu binafsi, mashirika na serikali ambazo zimeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na ubora wa maisha, sehemu mbali mbali za dunia.

Vatican inatambua matatizo na changamoto za kuwapokea na kuwahudimia wakimbizi na wahamiaji. Lakini changamoto zote hizi zinapaswa kushughulikiwa kwa kuambata haki inayomwilishwa katika huruma ya Mungu. Hii ni changamoto ya kisiasa na kijamii, lakini zaidi ni changamoto ya kimaadili na kiutu anakaza kusema Askofu mkuu Paul Richard Gallagher. Ukarimu na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni utambulisho makini wa taifa lolote lile kwa sasa na kwa siku za usoni. Mwaliko ni kufungua malango na mipaka ya nchi, ili kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwashirikisha tunu msingi za maisha ya kiutu zinazofumbatwa katika nchi wahisani na kwa njia hii, kweli dunia inaweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.